Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), imetoa hofu kuhusu idadi kubwa ya watoto waliotoweka barani Afrika baada ya kuchapisha ripoti juu ya Siku ya Kimataifa ya Kutoweka na kuonya kwamba zaidi ya watoto 25,000 wamepotea.
Idadi hiyo, inawakilisha asilimia 40 ya kesi 64,000 za watu waliopotea barani Afrika, kulingana na takwimu za ICRC ambayo inasema miongoni mwa masuala yanayosababisha upotevu huo ni pamoja na ukosefu wa usalama, kutokana na uwepo wa zaidi ya migogoro 35 ya silaha katika bara zima.
Hali hiyo, inatajwa kusababisha maelfu ya watu, wakiwemo watoto wanaovuka mipaka, jangwa la Sahara na bahari ya Mediterania kutafuta mahali salama na maisha bora, yatakayowaweka mbali na migogoro.
Harakati kama hizo, hubeba hatari kubwa na kutoweka ni juu ya orodha, na ripoti hiyo inasema, “Kwa bahati mbaya, kesi 25,000 zilizorekodiwa hazionyeshi ukubwa kamili wa shida hii ya kusikitisha na mara nyingi kupuuzwa ya kibinadamu kulingana na kamati.”
Aidha, Mkurugenzi wa kanda wa ICRC wa Afrika, Patrick Youssef anafafanua kuwa, “Hakuna shaka kwamba kuna watoto wengi zaidi ambao hawana habari kuwahusu, wakati wa safari zao, watoto wanakabiliwa na hatari kadhaa kama vile unyonyaji, vurugu, dhiki ya kisaikolojia na kutoweka.”