Takriban watoto 972 wameuawa au kujeruhiwa na ghasia tangu vita vilipoongezeka nchini Ukraine karibu miezi sita iliyopita, ikiwa ni wastani wa zaidi ya watoto watano wanaouawa au kujeruhiwa kila siku.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Catherine Russell kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis amesema “Takwimu hizi ni zile ambazo Umoja wa Mataifa umeweza kuthibitisha na tunaamini idadi ya kweli itakuwa ni kubwa zaidi.”
Ameongeza kuwa, “Matumizi ya silaha za vilipuzi yamesababisha vifo vingi vya watoto. Silaha hizi hazibagui raia na wapiganaji, hasa zinapotumiwa katika maeneo yenye watu wengi kama ilivyokuwa nchini Ukraine huko Mariupol, Luhansk, Kremenchuk, na Vinnytsia na rodha inaendelea.”
Hata hivyo, Russell amesisitiza kuwa kwa mara nyingine katika vita vyote maamuzi ya watu wazima ya kutojali, yanawaweka watoto katika hatari kutokana na kutokuwepo kwa operesheni za silaha za aina hiyo ambazo hazisababishi watoto kudhurika.
Ameongeza kuwa, “Mbali ya hofu zaidi ya watoto kuuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi, karibu kila mtoto nchini Ukraine amekabiliwa na matukio yenye kuhuzunisha sana, na wale wanaokimbia machafuko wako katika hatari kubwa ya kutengana na familia zao, kukabiliwa na ghasia, dhuluma, unyanyasaji wa kingono, na usafirishaji haramu wa binadamu.”
Aidha, Bi. Russell amefafanuwa kuwa wakati muda wa kurejea shuleni ukiwa umebakiza wiki moja, hatua hiyo pia inakumbusha ni kiasi gani Watoto wa Ukraine walivyopoteza masomo, na kwamba mfumo wa elimu wa Ukraine umesambaratishwa na kuongezeka kwa uhasama nchini kote.
“Shule zimekuwa zikilengwa au kutumiwa na pande zote katika vita na hivyo kusababisha familia kutohisi salama kupeleka watoto wao shuleni na tunakadiria kuwa shule 1 kati ya 10 imeharibiwa au kusambaratishwa,” amebainisha Russell.
Hata hivyo, mkuu huyo wa UNICEF amehitimisha taarifa yake kwa kutoa wito kwa pande zote katika mzozo nchini Ukraine kusitisha uhasama na kuwalinda Watoto wote dhidi ya vita hiyo ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi na kushambulia rai ana miundombinu.