Kampeni za uchaguzi Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC, zinakamilika rasmi hii leo huku tahadharishakuwa ghasia zinazohusiana na uchaguzi zinatishia uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Siku ya Jumatano Desemba 20, 2023.
Tahadhari hiyo, imetolewa na Shirika la Human Rights Watch kwa mamlaka za DRC kuchunguza kwa haraka na bila upendeleo matukio ya vurugu yanayohusiana na uchaguzi na kuwashtaki waliohusika, bila ya kujali wanaegemea upande gani wa kisiasa.
Mtafiti mkuu wa shurika hilo tawi la Congo, Thomas Fessy amesema, wameorodesha matukio kadhaa ya vurugu yaliyofanyika kote nchini humo kati ya wafuasi wa vyama hasimu vya kisiasa ambazo zimesababisha mashambulizi ya kulipa kisasi, unyanyasaji wa kingono na kifo cha mtu mmoja.
Zaidi ya watu milioni 1.5 hawataweza kushiriki zoezi la kupiga kura katika maeneo yenye mizozo, hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini na jimbo la magharibi la Mai-Ndombe na inadaiwa kuwa mamilioni ya wakimbizi wa ndani pia huenda wasishiriki zoezi hilo.