Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amepingana na Mashabiki wa Soka la Bongo wanaoendelea kumsifia Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison.
Zakazakazi amesema Kiungo huyo aliyesajiliwa Young Africans kwa mara ya pili akitokea Simba SC ni mchezjai wa kawaida, na haoni sababu ya Mashabiki kuendelea kumpa sifa kubwa.
Amesema Morrison amekua na kasumba ya kucheza michezo kadhaa vizuri na mingine anaboronda, hivyo hawezi kuwa mchezaji mwenye hadhi ya kupewa uzito mkubwa kiasi hicho.
“Morrison nyie mnampa hype kubwa sana, Morrison ni mchezaji wa kawaida tu, mchezaji ambaye ambaye anacheza vizuri baada ya Mechi tano, Msimu uliopita kacheza mechi ngapi? alafu ana goli moja tu, siyo kwa hype hii mnayompa, misimu miwili na nusu Tanzania hajafikisha magoli 10 sasa huyu siyo mchezaji wa kutaka kusema unatia watu,” amesema Zakazakazi
Awali Morrison alisajiliwa Young Africans misimu mitatu iliyopita, lakini miezi kadhaa baadae aliingia kwenye mzozo na viongozi wa klabu hiyo kwa madai ya mkataba feki, hatua ambayo ilimpa nafasi ya kutimkia Msimbazi mwanzoni mwa msimu wa 2020/21.
Mwishoni mwa msimu wa 2021/22, kiungo huyo alimalizana na Simba SC na kufanya maauzi ya kurejea Young Africans, hivyo msimu ujao wa 2022/23 atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha klabu hiyo ya Jangwani.