Mjadala wa Mshambuliaji kutoka DR Congo na klabu ya Young Africans Fiston Kalala Mayele kushindwa kutimiza ahadi yake ya kuifunga Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeendelea kuwa gumzo, huku kila mdau wa Soka la Bongo akisema na kuandika lake.
Mayele jana Juammosi (April 30), alishindwa kufurukuta katika safu ya ulinzi ya Simba SC iliyokuwa chini ya Henock Inonga na Joash Onyango, huku mshambuliaji huyo akipiga shuti moja lililokwenda nje ya lango la timu pinzani.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘ZAKAZAKAZI’ ni mmoja wa wadau wa soka waliojitosa na kuwa sehemu ya mdadala wa jambo hilo.
‘ZAKAZAKAZI’ ambaye aliwahi kuibua hoja baada ya mchezo wa Azam FC na Young Africans kuhusu Mayele, ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuandika ujumbe ambao unatoa ufafanuzi wa aina ya Washambuliaji wa soka duniani.
‘ZAKAZAKAZI’ ameandika: Kuna washambuliaji wa hadhi kuu nne.
Hatari sana.
Hatari.
Kawaida.
Chini ya kawaida.
Hatari sana.
Hufunga mabao sawa na idadi ya mechi walizocheza, na zaidi.
Yaani katika mechi 20, anafunga mabao kuanzia 20 na kuendelea.
Hatari.
Hufunga mabao sawa na robo tatu ya hadi sawa na idadi ya mechi alizocheza.
Yaani katika mechi 20, anafunga mabao kuanzia 15 hadi 20.
Kawaida
Hufunga mabao sawa na nusu ya mechi alicheza hadi robo tatu.
Yaani katika mechi 20, anafunga mabao kuanzia 10 hadi 15.
Chini ya kawaida
Hufunga mabao kuanzia moja hadi nusu ya mechi alizocheza.
Yaani katika mechi 20, anafunga mabao kuanzia moja hadi 10.