Imeandikwa na Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’
Katika moja ya kanuni za mpira ambazo zinabidi kufanyiwa mabadiliko ni usimamizi wa waamuzi.
Badala ya kuwa chini ya mamlaka za mpira, iruhusiwe kuwa chini ya makampuni au taasisi binafsi ambazo zitakuwa zikiwakodisha kwa mamlaka za mpira.
Makampuni yatashindana kutengeneza waamuzi bora na wenye ushindani ili kutoa huduma nzuri hivyo kuliteka soko.
Kampuni itakayokuwa na waamuzi bora na kutoa huduma nzuri ndiyo itakayopewa mechi nyingi hivyo kufanya biashara kubwa.
Na kuwe na kipengele kwenye mkataba wa zabuni kwamba endapo mwamuzi ataharibu mchezo kwa makosa ya uzembe, kampuni yake ilipe gharama ambazo klabu iliyoathirika imezipata.
Makosa ya uzembe ni yale yale ambayo kwa sasa yanatumika kuwafungia waamuzi.
Ni kama ilivyo kwa mikataba ya makampuni ya ulinzi, ukitokea upotevu kwenye lindo fulani na uchunguzi ukibaini ulitokana na uzembe wa askari, kampuni iliyopewa dhamana inalipa.
Kama inawezekana kutoa zabuni kwa makampuni binafsi ya ulinzi kusimamia usalama wa mali na maisha ya watu, kwanini isiwezekane kwa waamuzi wa mpira?
Bila hivyo kila siku tutakuwa tunawatumia waamuzi wale wale kwa sababu ndiyo waliopo na hawana wanayeshindana naye.
Hata anayewasimamia na kuwaandaa hana presha ya kukosa soko kwa sababu anajua hata wakiwa na kiwango cha chini kiasi gani watatumika tu kwa sababu hakuna mbadala.
Wakati Posta na Simu ilipokuwa kampuni pekee ya mawasiliano Tanzania, huduma ilikuwa chini sana.
Lakini yaliporuhusiwa makampuni binafsi ya simu, huduma ikaimarika na kufika kila kona ya nchi.
Kukiwa na makampuni binafsi yanayosimamia waamuzi, inawaajiri na kuwalipa mishahara, itasaidia sana kuyabana ili yatoe huduma bora.
FIFA, CAF na IFAB yaache ukiritimba…yafungue milango kwa taasisi binafsi kusimamia waamuzi…wao hii kazi imewashinda!