Mkuu Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam Azam FC Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema hawana shaka na mchezo dhidi ya Young Africans ambao watawakabili katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi April 06.
‘Zakazakazi’ amesema mchezo huo ni wa kawaida kama ilivyo michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo wanajiandaa katika hali ya kawaida.
Amesema baadhi ya Wadau wa Soka wamekua wakihisi Azam FC wanauhofia mchezo huo, lakini ukweli ni kwamba Uongozi, Benchi la Ufundi na Wachezaji wanajipanga katika hali ya kawaida ili kutimiza lengo la kupambana na kupata matokeo chanya.
“Mchezo wetu unaofuata Azam FC ni dhidi ya Young Africans utakuwa wakawaida na wala hatuutolei macho kwani wametuzidi alama nyingi sana kwenye msimamo wa Ligi Kuu , Kwa hiyo hata tukishinda Mchezo huo au kupoteza haitatusaidia kitu” amesema ‘Zakazakazi’
Katika hatua nyingine ‘Zakazakazi’ amesema hawatishwi na Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele ambaye kwa sasa ndio habari kubwa katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema Azam FC imewahi kukutana na Washambuliaji hatari Barani Afrika akiwemo Ramadan Sobi wa Pyramid FC na hakufurukuta, hivyo Mayele ni mchezaji wa kawaida sana kwao.
“Sisi hatumuogopi Fiston Mayele kwakuwa tulikutana na wachezaji wakubwa zaidi yake kama Ramadan Sobi wa Pyramids lakini kufurukuta, Mayele ni wa kawaida sana ama kuwa anacheza timu yenye mashabiki wengi ndio maana anaimbwa sana, ana magoli 9 tu, Masikini akipata?”
Azam FC inakwenda kukutana na Young African April 06, ikiwa imejikusanyia alama 28 zinazoiweka nafasi ya 03 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Wananchi wakiwa kileleni kwa kufikisha alama 48.