Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu uwezo na ujio wa Kiungo Mshambuliaji Abdul Seleman Sopu.
Azam FC imekamilisha usajili wa Mchezaji huyo jana Jumatatu (Julai 04), baada ya kuvutiwa na uwezo wake kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ uliochezwa Jumamosi (Julai 02) dhidi ya Young Africans jijini Arusha.
Zakazakazi amesema Sopu sio mchezaji wa kaiwada, kutokana na uwezo wake kuwa wazi kwa wadau wa soka nchini Tanzania, baada ya kuonyesha hivyo kwenye michuano ya ASFC.
Amesema Azam FC imeonyesha na kutambua uwezo wa Mshambuliaji huyo, na ndio maana imepambana kumsajili na kufanikiwa kutoka midomoni mwa klabu Kongwe nchini Tanzania Simba SC na Young Africans ambazo zilitajwa kuiwania saini yake saa chache baada ya mchezo wa Fainali ya ASFC.
“Sopu sio mchezaji wa kawaida, amefunga hat trick kwenye fainali dhidi ya timu yenye ukuta imara. Sopu ni zaidi ya mchezaji wa kawaida ‘extraordinary’.” amesema Zakazakazi
Abdul Sopu amejiunga na Azam FC akitokea Coastal Union ya jijini Tanga kwa dau linalotajwa kufikia Shilingi milio 100.