Mkurugenzi wa Timu ya African Lyon iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kuanzia msimu ujao, Raheem Kangezi Zamunda ametangaza rasmi kuachana na masuala ya soka.
Zamunda ambaye ndiye mmiliki wa timu hiyo kwa kipindi cha takriban miaka saba, amesema sababu kubwa ya kufikia uamuzi huo ni matatizo na vikwazo anavyodai kukutana navyo katika ulingo wa soka la Tanzania.
Amesema kwa kipindi chote ambacho amekuwa mdau wa soka nchini, amekuwa na mchango mkubwa lakini wapo watu ambao hajawaweka hadharani wamekuwa wakikwamisha jitihada zake, huku mchango wake ukiwa hauthaminiwi.
Amesema ameamua kuacha kabisa masuala ya soka ndani ya nchi na atazungumzia hatma ya African Lyon siku chache zijazo ambapo amepanga kuwaachia kile alicho.
“Sekta ya soka Tanzania ni ngumu sana, ina matatizo mengi sana… Nilichojifunza kwa miaka saba nitawaachia vijana ili waelewe ugumu uliopo… Mtu unamdhamini kwenye ubalozi, halafu ‘hater’ mmoja anakwenda kuzungumza ujinga… Nitaongea na waandishi wa habari kuhusu hatma ya timu na kama nitaiuza,” hiyo ni sehemu ya kauli ya Zamunda wakati akizungumza na kituo kimoja cha radio nchini.
African Lyon ni moja kati ya timu sita ambazo zimepanda daraja kujeza ligi kuu msimu ujao, timu nyingine zikiwa ni JKT Tanzania, Coastal Union, Alliance, Biashara United na KMC.
Tangu timu hiyo ichukuliwe na Zamunda akiibadilisha jina kutoka Mbagala Market na kuwa African Lyon, imekuwa ikipanda na kushuka kutoka ligi kuu.