Timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rwanda kwenye mchezo wake wa kwanza Kundi A michuano ya CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya.

Zanzibar ambayo imetandaza kandanda safi na la kuvutia ilifanikiwa kuandika bao la kuongoza dakika ya 35 kipindi cha kwanza kupitia kwa Abdu-Aziz Makame ambaye alimalizia kwa kichwa krosi nzuri ya Mudathir Yahya. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Aidha, kipindi cha pili Rwanda ilianza kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 47 kupitia kwa kijana Hakizimana Niyonzima ambaye ni mdogo wake na nyota wa Simba Haruna Niyonzima.

Bao la pili la Zanzibar limefungwa na Mohammed Juma dakika ya 52 huku bao la tatu likifungwa na Kassim Khamis dakika ya 86. Matokeo hayo sasa yanaiwezesha Zanzibar kushika nafasi ya pili katika kundi A nyuma ya Kenya.

Hata hivyo, Zanzibar Heroes itacheza mchezo wake wa pili na ndugu zao wa Kilimanjaro Stars siku ya Alhamis Desemba 7. Kilimanjaro ilitoka sare ya bila kufungana na timu ya taifa ya Libya kwenye mchezo wa kwanza.

 

Mgodi wa GGM wang'ara mashindano ya SHIMMUTA
Mbaraka Yusuf kuwakosa Zanzibar Heroes