Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu mbali mbali kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.
Ameyasema hayo Chake-Chake wakati akiwatunuku vyeti wahitimu 167 wa chuo cha elimu ya biashara na uongozi (ZCBE) kwenye sherehe za mahafali ya pili ya chuo hicho kisiwani Pemba, amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuwekeza katika elimu kwa vijana wao kwani rasilimali za nchi haziwezi kutumika vizuri bila ya kuwa na vijana waliobobea kitaaluma na wananchi walioelimika.
“Serikali inaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu kwa lengo la kukuza uchumi , hivyo ni vyema vijana mtakaokabidhiwa vyeti hii leo kuzitumia fursa zilizopo kuweza kujiajiri wenyewe ”amesema Dkt Khalid.
Aidha, amewanasihi wahitimu hao wasibweteke na kusubiri ajira kutoka serikalini na badala yake watumie ujuzi na maarifa waliyoyapata kubuni njia za kujiajiri wenyewe ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi wa ushirika na ujasiriamali
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho , Abdulwahab Said Bakari amaeiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikiria uwezekano wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya cheti na diploma kwani vijana wengi wanashindwa kujiendeleza kutokana na kukosa ada za malipo.
Hata hivyo, wahitimu wa chuo hicho wamezitaka taasisi kuondoa vikwazo vya uzoefu wakati wanapotangaza nafasi za kazi ili kuwafanya vijana wanaomaliza vyuo kupata nafasi za kuajiriwa