Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inaendelea na vikao vya ushirikiano baina yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhakikisha Zanzibar wa Tanzania inapata uanachama kamili katika Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati akijibu swali la Profesa Omar Fakih Hamad Mwakilishi wa Jimbo la Pandani aliyetaka kujua Serikali imefikia wapi katika suala la Zanzibar kujiunga na kujitegemea katika michuano ya kimataifa.
Akijibu swali hilo, Waziri Tabia amesema kupitia wizara yake inaendelea kufanya jitihada hizo na kwamba kwa sasa Zanzibar ni mwanachama wa Shirikisho la Soko la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Waziri huyo amesema kwa upande wa ujenzi wa viwanja vya michezo kupitia wizara hiyo imekamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya wilaya vinne vitakavyoanza kujengwa katika Wilaya ya Chakechake na Wilaya ya Micheweni Pemba.
Amesema hatua za ujenzi zitaanza baada ya kukamilisha mikataba. Pia, Waziri huyo amesema wizara yake imefunga mkataba na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vinne vya Unguja na Pemba.
Akijibu swali la kuhusu utaratibu wa kuandaa mitaala ya mafunzo kwa viongozi wa vyama vya michezo Waziri huyo amesema serikali kupitia wizara yake haina mtaala rasmi wa kufundisha mambo ya michezo.
“Wizara inatarajia kuandaa mtaala wa michezo katika bajeti ya mwaka 2024/25 na kwa sasa inaendelea na taratibu za kuandaa wasimamizi wa mtaala huo mara tu utakapokamilika.
Hata hivyo, Wizara kupitia Idara ya michezo na Baraza la Michezo Zanzibar hufanya mafunzo kwa viongozi wa vyama vya michezo kwa kutumia wakufunzi kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema
Katika maelezo yake Waziri huyo amesema Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kinatoa Stashahada ya Elimu ya Sayansi ya Michezo ambapo moja ya kozi zake ni Uongozi na Uendeshaji wa michezo.