Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza hatua za Serikali ya Ujerumani za kurudisha uhusiano na ushirikiano wa kimaendeleo kati yake na Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika salamu zake za shukrani kwa Serikali ya Ujerumani kwa hatua yake ya kurudisha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar wa muda mrefu utakuwa wa kimaendeleo, uhusiano ambao ulisitishwa na nchi hiyo ya Ujerumani tokea mwaka 2015.
Alisema kuwa kurudisha mashirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani kutaimarisha maendeleo hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar katika visiwa vyake vyote vya Unguja na Pemba.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Ujerumani ina historia kubwa ya kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar na pia, ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wake na kusaidia Zanzibar tokea mwaka 1965 ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makaazi, maarufu nyumba za Mjerumani zilipo Kikwajuni Mjini Zanzibar, nyumba za maendeleo za Bambi, kusaidia maendeleo ya Mji Mkongwe Zanzibar pamoja na kusaidia huduma mbali mbali za kijamii.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi, alisema kuwa kurejesha uhusiano huo wa maendeleo haupo kimaneno badala yake uko kivitendo kwani tayari Ujerumani imeshakusudia kusaidia kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo miradi kadhaa ya maendeleo kama vile miradi ya maji, afya, michezo pamoja na kuunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu.