Siku ya kina baba dunia kwa mara ya kwanza ilianzishwa na mwanamke mmoja raia wa Marekani aliyejulikana kwa jina la Sonora Smart Dodd aliyelelewa na baba pekee ambaye aliwalea yeye na wenzake watano hivyo alihamasika kuanzisha siku hiyo mara baada ya kuona namna ambavyo raia wa nchi hiyo wanavyosherekea siku ya kina mama duniani ambayo hufanyika Mei 13 kila mwaka.
Kwa mara ya kwanza siku ya kina baba duniani ilifanyika huko nchini Marekani Mji wa Washington mnamo june 19, 1910 na siku hii huenda kwa kubadilika kila mwaka na mwaka huu inatarajiwa kuadhimishwa Juni 17.
Kuelekea siku hii zifuatazo ni zawadi ambazo mama, mtoto au rafiki anaweza kufikiria kumpa mwanababa kama heshima ya kuwa baba bora na mwenye mchango mkubwa katika familia na pia kuonesha jinsi ambavyo unaithamini siku hiyo.
- Pochi nzuri yenye rangi ya bluu iliyopoa kwa ajili ya kuhifadhi vitu kama pesa, vitambulisho na n.k ambayo itaendana vyema na suti atakayoamua kuipigilia siku hiyo.
- Manukato, wababa wengu hupuuzia vitu ambavyo kwao wanaona havina faida yeyote, siku hii unaweza kumzawadia baba manukato yenye harufu nzuri kuonesha unajali muonekano wake na unadhifiu wake kwani harufu nzuri huchangia kuonekana nadhifu.
- Soksi jozi tano, wanaume wengi ni wavivu kununua vitu vidogo vidogo kama soksi, leso, nguo za ndani kama vile vesti na n.k hivyo kwa kumnunulia soksi jozi tano ni namna moja wapo ya kuonesha unamjali katika siku hiyo muhimu.
- Saa ya ngozi, pia unaweza kumtunuku baba zawadi ya saa nzuri ambayo una uhakika ataifurahia ili kumuwezesha kutunza muda wake na kufanya mambo kwa wakati.
- Mkanda kwa ajili ya kuvalia suruali zake pindi anapotoka kuelekea kazini.
Hivi ni vitu vidogo lakini vina maana kubwa sana hasa unapompa mtu kama zawadi, mbali na hivyo kuna vile vitu ambavyo unajua kama ni baba yako au mume huwa anavipenda ila anakosa muda wa kuvinunua au kuvifanya hii ndio siku ya kumfurahisha baba au mume katika siku yake hii muhimu.
Japokuwa wanawake wengi wa kitanzania wamezoa kupokea tu zawadi kutoka kwa wakina baba basi dunia imewaandalia siku kina mama nao kuwanunulia zawadi kina baba katika siku yao muhimu, hivyo ni vyema kuiadhimisha vizuri.