Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), imetakiwa kuangalia pengo la Kisera katika mfumo wa ukusanyaji mapato nchini na kuufanyia mageuzi sahihi, ili kuongeza ufanisi na kukuza kiwango cha mapato Zanzibar.
Hayo, yamebainishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman mjini Zanzibar, katika mazungumzo na Kamshina wa ZRB, Ramadhani Juma Mwenda kuhusu namna ya kuchangia ufanisi na kukuza kiwango cha mapato Zanzibar.
Amesema, “yapo maeneo mengi ya mapato ambayo yanaweza kufanyiwa mageuzi ya kisera na kisheria jambo litakalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa kupitia vyanzo tofauti vilivyopo nchini.”
Othman ameongeza kuwa, ipo haja ya kuchambua zaidi viwango vya malipo vinavyokana na ushuru wa stamp, hasa katika kutafautisha mapato ya aina hiyo kupitia miradi mikubwa na inayoanzishwa nchini ile ya kawaida ambapo viwango vyake vinaweza kuwa tafuati kuliko ilivyo sasa.
Kwa upande wake, Kamshida wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Ramadhani Juma Mwenda, amesema wanaendelea kufanya mageuzi katika mifumo ya ndani ya ukusanyaji mapato jambo linalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa Zanzibar kupitia bodi hiyo.
Amesema, kutokana na hali hiyo wamefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 131 hadi 135 kwa kipindi cha miezi mitatu.