“AZAM MPYA INAKUJA” Hiyo ndiyo kauli ya makocha wapya wa benchi la ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, ambao tayari wameshaanza kazi rasmi tokea Alhamisi iliyopita kujiandaa na msimu ujao (2016-17).

Benchi hilo chini ya makocha kutoka nchini Hispania, linaongozwa na Zeben Hernandez, Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia na Msaidizi wake, Pablo Borges na Kocha wa Makipa Jose Garcia huku Daktari wa timu, Sergio Perez, akitarajia kutua nchini muda wowote kuanzia sasa.

Wataalamu hao wataongezewa nguvu na makocha wengine wazawa waliokuwepo na kikosi hicho msimu uliopita, Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na Idd Abubakar, aliyekuwa akiwapata maujuzi makipa wa Azam FC.

Wakati timu hiyo ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya ikifikisha siku ya tano leo Jumatatu, mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz umepata fursa ya kufanya mahojiano maalumu na Kocha Mkuu Zeben, ambaye ameeleza namna alivyojipanga kuijenga Azam FC mpya itakayocheza soka la kisasa.

Na yafuatayo ni mahojiano hayo;

Unajisikiaje wewe na benchi lako la ufundi kupata nafasi ya kuinoa Azam FC?

Tunafuraha kubwa kupewa nafasi ya kufanya kazi hapa, Azam FC ni timu nzuri na tumefurahia miondombinu ya timu, pia watu wa hapa wamejipanga, kikubwa kila mtu yupo tayari kufanya kazi vema na kwa bidii kwa ajili ya kuleta mabadiliko Azam FC, ambayo tutaitengenezea falsafa mpya na kuifanya kuwa timu kubwa Afrika,” alisema.

Umekionaje kikosi cha Azam FC kwa ujumla?

Kocha huyo wa zamani wa Club Deportivo Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa amefurahishwa na ubora wa wachezaji wote wa Azam FC baada ya kuwaona akiwa kwenye mazoezi yanayoendelea na vilevile katika mechi mbili dhidi ya African Sports (1-0) na Mgambo JKT (1-1) msimu uliopita.

“Ninachoshukuru ni kwamba wachezaji wote wapo vizuri, wanajituma na pia wana vipaji, ila tuna kazi kubwa hapo mbeleni na lengo letu tunataka Azam kama klabu kuwa na furaha na yenye kuridhisha mashabiki wake, kwa sasa tnafanya tathimini ya wachezaji ili kufanya maamuzi nani atabakia na nani ataondoka, ingawaje utakuwa ni wakati mgumu kwa wachezaji ila hatuna budi kutekeleza,” alisema.

Mashabiki wengi wa Azam FC hivi sasa wanajiuliza umekuja na aina gani ya soka, Je, unapenda kuwaambia nini?

“Mashabiki watarajie soka zuri la pasi lenye kuvutia pamoja na matokeo mazuri, malengo yetu ni kuifanya Azam FC kwenye msimu ujao iwe ni timu ya ushindani na tunataka tuione mwakani ikipanda kimpira na kuwa timu bora barani Afrika.

“Ninachoamini muda mchache ujao Azam itakuwa bora na mchezo wa uwanjani utakuwa mzuri, njia zetu na mbinu za ufundishaji zitakuwa ni bora kabisa Tanzania, hayo ni mambo muhimu kabisa kwa Azam,” alisema.

Kila kocha huamini katika mifumo yake, vipi kwa upande wako ni mifumo ipi hupendelea timu yako kucheza?

“Mimi huwa napendelea soka la pasi, wachezaji kucheza kwa kasi wakiwa na mpira pamoja na kukaba haraka pale tunapokuwa hatuna mpira, timu kucheza kwa uelewano na kitimu, mfumo nitakaoutumia Azam FC kwa ajili ya kucheza soka safi ni 4-3-3 na mbadala wake ni 4-2-3-1, ni sawa sawa na staili wanayocheza Barcelona.

“Kwenye mfumo huo ni jambo zuri kuwa na mabeki wanne wazuri nyuma na wachezaji wengine watatu katika mstari unaofuata kwenye kiungo watakaokuwa katika nafasi tofauti, na kwenye mstari wa mwisho kutakuwa na wachezaji wengine watatu, wawili pembeni na mshambuliaji mmoja atakayesimama mbele,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Jambo kubwa kwangu ni kushambulia, nahitaji mabeki wawili wa pembeni wenye uwezo mkubwa wa kushambulia na kasi, viungo wa kati wenye uhodari wa kushambulia, na katika wachezaji watatu waliokuwa mbele, wawili nao watakuwa wakishambulia na kumsaidia mshambuliaji mmoja atakayekuwa akisimama mbele katikati. Mfumo wa 4-2-3-1 nitautumia kulingana na aina ya mpinzani tutayekutana naye.”

Barcelona ambayo ni klabu bora kwa sasa iliyofanikiwa zaidi kuliko timu yoyote kwa miaka 10 hii ulimwenguni, imepata umaarufu mkubwa na mafanikio kupitia falsafa yake ya uchezaji inayoitwa ‘tik-tak’, inayohusisha soka la burudani linalowafanya wachezaji muda mwingi kumiliki mpira kwa kupigiana pasi nyingi kwa kasi, aina ya soka ambalo limekuwa likizisumbua timu nyingi zinazocheza nazo.

Soka la pasi linachezwa kiufasaha kwenye viwanja bora, Je umejipangaje kukabiliana na viwanja vibovu nchini?

Baada ya kuja nchini kwa mara ya kwanza, Zeben aliishuhudia Azam FC ikicheza dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambao hauko vizuri, ambapo amesema amejipanga kukabiliana na hali hiyo.

“Nimeshagundua ubovu wa baadhi ya viwanja hapa, nitatumia mfumo mwingine badala ya kucheza mipira mirefu tu kwenye viwanja hivyo, tutacheza pasi, pasi, pasi kadhaa kwa haraka kisha tutapiga mpira mrefu, tukifanikiwa kuupata mbele tutapasiana tena na kumalizia shambulizi langoni kwa kufunga,” alisema Zeben mwenye leseni ya juu ya ukocha ya Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA Pro Licence).

Ulibahatika kushuhudia michuano ya vijana ya Azam Youth Cup 2016 ukiwa nchini Hispania, Je, umeionaje Azam FC Academy iliyoibuka mabingwa?

“Nilikuwa nikiifuatilia ile michuano, nimefurahishwa nayo sana, Azam Academy ni timu nzuri, kuna baadhi ya wachezaji wanavutia sana kwa mfano namba 43 (Shaaban Idd), 40 (Rajabu Odas) na 34 (nahodha Abdallah Masoud),” alisema na kudai kuwa wanamfaa kuchezea timu ya wakubwa, ambapo hivi sasa anaendelea kuwaangalia kwenye mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya yanayoendelea kwenye dimba la Azam Complex.

Makocha hao wanatua nchini kuziba nafasi za benchi la ufundi lililopita chini ya Mwingereza Stewart Hall, Msaidizi wake Mario Marinica na Mtaalamu wa Viungo, Adrian Dobre (wote kutoka Romania), waliojiuzulu kuinoa timu hiyo mara baada ya mchezo dhidi ya JKT Ruvu (2-2) msimu uliopita, lakini waliondoka rasmi mara baada ya Azam FC kuichapa African Sports.

Chanzo: Azamfc

Mionekano ya Mastaa wikiend hii
Antoine Griezmann: Sina Furaha Na Tuzo Ya Ufungaji Bora