Shirikisho la Soka Visiwani Zanzibar ‘ZFF’, limepanga kukutana na viongozi wa timu za KMKM na JKU ili kujua mikakati yao katika michuano Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Rais wa ZFF, Suleiman Jabir amesema mazungumzo ya Shirikisho lake na viongozi wa klabu hizo yana nia ya kuhakikisha wawakilishi hao wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika wanafanya vizuri
Jabir ameongeza kuwa timu ya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), ambao ni mabingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Zanzibar wataviwakilisha visiwa hivyo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Mara tu baada ya kuingia madarakani katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni, tumepanga kuzungumza na viongozi wa klabu zetu za KMKM na JKU. Lengo letu ni msimu huu ni kuziunga mkono kabu hizo, ili walau zikacheze hatua ya makundi na siyo vinginevyo,” amesema rais huyo.
Pia, amesema michuano ya Ligi Kuu ya Zanzibar, msimu ujao imepangwa kuanza Septemba 9, mwaka huu ambapo timu zitakazoshiriki zitaruhusiwa kusajili wachezaji tisa wa Kigeni.
Rais huyo, amesema hatua hiyo imelanga kuziimarisha zaidi klabu za soka za kisiwani humo, ili zipate uwezo wa kushindana Kimataifa na klabu zingine barani Afrika.
“Naamini huu ni mwanzo tu, tumeanza na kuruhusu klabu za ligi kusajili wachezaji tisa wa kigeni, ZFF itaendelea kufanya mabadiliko na kanuni mbalimbali, tunahitaji kufanya maboresho zaidi ili iweze kuwa na ushindani mkubwa,” amesema Rais wa ZFF
Wakati timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi ‘JKU’, wataiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, KMKM imepangwa kuanza katika Raundi ya awali, Agosti 18, mwaka huu itacheza na timu ya Kedus Giorgis, wakati JKU watacheza raundi hiyo dhidi ya Singida Fountain Gate ya Tanzania Bara.