Mwanamuziki kutoka nchini Ukraine Zi Faamelu, aliyebadili jinsia yake kutoka mwanaume na kuwa mwanamke, amezilalamikia mamlaka nchini humo baada ya kuzuiliwa kutoka nje ya mipaka ya Ukraine kwa kuwa pasipoti yake ya kusafiria inaonyesha yeye ni mwanaume.
Zi Faámelu ambaye ana umri wa miaka 31 anasema kuwa sehemu ya jinsia kwenye pasipoti yake bado inaonyesha kuwa yeye ni mwanamume na mamlaka ya mipaka ya Ukraine haikumruhusu kupita ikiwa ni sehemu ya kufuata agizo la rais wa nchi hiyo kuwa wanaume wote hawapaswi kutoka nje ya nchi hiyo ili kuipigania nchi yao.
Kwa mujibu wa ripoti, mamia ya watu wanaosafirishwa wamekwama kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo kwa kuwa hati zao za vitambulisho bado zinaonyesha wao ni wanaume.
Inaelezwa kuwa ni kuna ugumu kwa watu wa Ukraine waliobadili jinsia na kuwa wanawake kupata upenyo wa kutoka nje ya Ukraine kutokana na pasipoti zao kushindikana kubadilishwa kwenye kipengele cha jinsia hivyo kuendelea kutambulika kama wanaume.
Kwa mujibu wa Human Rights Watch, mara nyingi watu hao wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili na upasuaji wa kuthibitisha jinsia ili kusasisha (ku-update) hati zao rasmi.
“Hii ni kama, kuufedhehesha ulimwengu…Niliamua kuweka mwanamume kwenye pasipoti yangu, na sasa siwezi kuondoka katika nchi hii. Saa chache zilizopita nilisikia milipuko ya mabomu na madirisha yangu yakitetemeka, ninaogopa sana maisha yangu, niko peke yangu sasa. Kila mtu hasa majirani zangu wameondoka. Ni hali ya hatari sana, lakini ninajaribu kuwa na matumaini.” Zi Faámelu aliwaambia waandishi wa habari.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamewashauri baadhi ya watu wanaovuka mipaka kutupilia mbali pasipoti zao ili watoke nje ya Ukraine.
Kulingana na takwimu za UNHCR, zaidi ya raia milioni 1 wa Ukrainia wamekimbia nchi tangu vita vilipoanza Februari 24, 2022. Shirika hilo liliongeza kwamba “idadi hii imekuwa ikiongezeka sana, saa baada ya saa.”