Ziara ya kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya (NASA), Raila Odinga kutembelea nyumbani kwa rais wa zamani wa Kenya, Daniel Moi imekuwa gumzo nchini humo huku kukizuka mijadala mbalimbali wengi wakisema kuwa hiyo ni mikakati mipya ya maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2022 nchini humo.
Ziara hiyo imekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu kupita mara baada ya Raila Odinga kukutana na Rais, Uhuru Kenyatta kufanya mazungumzo na kuahidi kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuunganisha taifa hilo.
Aidha, wakati wa ziara hiyo, Odinga aliongozana na Seneta wa Vihiga, George Khaniri na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir.
Hata hivyo, ziara hiyo ilizua hisia na mijadala mikali katika mitandao ya kijamii nchini Kenya huku wengine wakiikashifu na wengine kuiunga mkono na kupongeza hatua hiyo.