Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa nchini India kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023 kufuatia mwaliko wa Droupadi Murmu, Rais wa Jamhuri ya India.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema ziara hiyo ya kimkakati imelenga kufanikisha mambo muhimu ya kiuchumi na kijamii yenye manufaa makubwa kwa Tanzania.
Amesema, “miongoni mwa mambo hayo kuongeza masoko ya mazao yanayozalishwa nchini na kuuzwa India kama vile mbaazi na korosho, kuanzishwa kwa kiwanda cha kutengeneza chanjo za wanyama na binadamu zenye ubora wa kimataifa;kuanzishwa kwa viwanda vya simu janja hapa Tanzania, kuanzishwa kwa taasisi ya upandikizaji wa Figo nchini.”
Ziara hiyo, itakuwa ya kwanza kufanywa na Rais wa Tanzania nchini India katika muda wa miaka minane iliyopita na zaidi ya wafanyabiashara 80 wa Tanzania watafuatana na Rais katika ziara hiyo huku Serikali za Tanzania na India zikitarajia kuingia mikataba ya ushirikiano 15 katika maeneo tofauti.