Gwiji wa soka nchini Brazil, Arthur Antunes Coimbra Zico, amewashutumu maafisa wa shirikisho la  soka duniani FIFA, kwa kusema wamekua wakijitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuwazuia wanasoka shupavu kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa shirikisho hilo.

Zico, ametupa shutuma hizo FIFA, baada ya kuona huenda akafungwa na kifungu cha kanuni za uchaguzi wa shirikisho hilo, ambacho kinawataka wagombea kuwasilisha barua ambayo imeambatana na taarifa za kuungwa mkono na mashirikisho ya soka ya nchi wanachama yasiyopungua matano miezi minne kabla.

Zico, amesema kanuni hiyo haina malengo mazuri na manguli wa soka duniani kama ilivyo kwake, na anaamini huenda imewekwa makusudi ili kuwabeba baadhi ya watu ambao tayari wameshajijengea wigo mpana katika mashirikisho ya soka ya nchi wanachama wa FIFA.

Amesema kulukua na umuhimu kwa wagombea kupewa nafasi ya moja kwa moja kuingia kwenye kinyang’anyiro na kufanyiwa maamuzi ya wapiga kura katika mkutano mkuu wa FIFA, na si utaratibu uliopo sasa ambao kwake anaamini unaendelea kutoa mwanya wa ufisadi ambao unalitafuna shirikisho la soka duniani kwa sasa.

Zico, alishaweka wazi atawania nafasi ya urais kwa kutangaza nia siku chache baada ya rais wa sasa Sepp Blatter, kutangaza ataachia nafasi yake February 26 ambapo uchaguzi mkuu wa FIFA utafanyika.

Maria Sarungi Awashangaa Chadema...
Pato: Nilikataa Kurudi Ulaya