Raia wa Zimbabwe wamefanya ibada ya kuiombea amani nchi yaio ikiwa ni muda mchache kabla ya uchaguzi wa kitaifa wa Agosti 23 unaotarajiwa kuwa na mvutano mkubwa huku kukiwa na ukandamizaji dhidi ya upinzani na mashaka ya wizi wa kura.
Idadi kubwa ya waumini, ilikusanyika kwa ajili ya misa katika kanisa lililopo katika barabara isio na lami na kuzungukwa na vibanda vya soko katika kitongoji kikongwe zaidi cha jiji la Harare cha Mbare.
Mchungaji wa kanisa hilo lenye kufahamika kama Apostolic Faith Mission, Edson Mukaro amenukuliwa akisema “Tunaombea mazingira ya amani. “Tunawahimiza tu, watu wetu kuwa watulivu, amani, na kufanya kila kitu kwa utaratibu.”
Zimbabwe ina historia ndefu ya chaguzi zenye mzozo zilizokumbwa na ghasia, na baadhi wanahofia kurudiwa kile kilichotokea mwaka wa 2018,pale ambapo jeshi lilipowafyatulia risasi waandamanaji wa upinzani, na kusababisha vifo vya watu sita.
Siasa na dini mara nyingi hufungamana katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, ambako makanisa ya yanatawala na rekodi zinaonesha baadhi ya viongozi wa kidini katika miaka ya nyuma waliegemea upande wa chama tawala cha ZANU-PF, ambacho kimekuwa katika hatamu ya uongozi tangu uhuru wa taifa hilo mwaka 1980.
Kwa mujibu wa AFP, Mukaro anasema jengo la kanisa la “Gospel Fire Cathedral”, lenye madirisha ya vioo na dari ya mbao, linahusika tu na mambo ya kiroho, si ya kisiasa. Anasema ” Sisi sio wafuasi wa kisiasa.”
Takwimu za serikali ya Zimbabwe zinaonesha zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaishi katika umasikini uliokithiri na upatikanaji wa ajira pia ni changamoto kubwa. Lakini katika eneo hilo ambalo kijadi lina ushawishi wa ZANU-PF muumini Anna Mukudo anasema “Tunahitaji ajira zaidi.“ Anasema ana matumanini uchaguzi ujao wa Agosti 23 utaleta mabadiliko na maboresho.