Serikali ya Zimbabwe imeeleza kukerwa na hatua ya Marekani kumwekea vikwazo balozi wake nchini Tanzania, Anselem Nhamo Sanyatwe.

Vyanzo vya habari nchini humo vinaeleza kuwa serikali ya Zimbabwe imeitaja hatua hiyo ya Marekani kama inayokandamiza uhuru wa taifa hilo.

Imesema kuwa hatua hiyo ya Marekani itapelekea mgawanyiko mkubwa ndani ya taifa hilo badala ya kuleta suluhisho la kitaifa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya Balozi Sanyatwe, ambaye ni Bregadia mstaafu wa jeshi la kitaifa la ulinzi wa rais, kutokana na kuhusika kwake na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Aidha, balozi huyo anadaiwa aliongoza operesheni maalum ambayo ilitumia nguvu ya ziada kuwakandamiza waandamanaji wakati wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 1 mwaka 2018 baada ya uchaguzi mkuu, uliosababisha vifo vya raia sita

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imempiga marufuku balozi huyo kuingia Marekani, ambapo Sanyatwe alikuwa kiongozi wa kikosi maalum cha kijeshi cha kumlinda Rais, lakini  kwasasa ni balozi wa Zimbwe nchini  Tanzania.

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na makundi ya kidini jana yaliadhimisha mwaka mmoja tangu wanajeshi walipofanya mauaji ya waandamanaji waliokuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi Julai mwaka jana.

Makundi yote yaliyoshiriki yalisema kuwa yataendelea kuomba Mungu aingilie kati taifa hilo la kusini mwa Afrika ambalo limekumbwa na ghasia kwenye mfumo wake wa kisiasa.

 

Serikali ya Msumbiji na wapinzani wasaini mkataba wa Amani
Nissan yatoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum