Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amewasilisha ombi rasmi ili nchi hiyo ijiunge tena na Jumuiya ya Madola baada ya kujitoa mwaka 2003, wakati wa utawala wa Robert Mugabe.
Zimbabwe ambayo ilitawaliwa na Uingereza, ilijitoa kwenye Jumuiya ya Umoja wa Madola baada ya Mugabe kutupilia mbali ukosoaji wa sera zake za kuwanyang’anya raia wa kigeni mashamba na kuwagawia wazawa pamoja ukosoaji mkubwa juu ya mfumo wa uchaguzi. Ukosoaji huo ulikuwa na shinikizo zaidi kutoka Uingereza.
Katika kuhakikisha uhusiano wa Zimbabwe na Jumuiya ya Madola unarejea kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2003, Rais Mnangagwa amewakaribisha waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya hiyo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Jenerali Patricia Scotland amesema kuwa Mnangagwa ambaye alichukua nafasi ya Mugabe Novemba mwaka jana, aliwasilisha barua hiyo ya maombi Mei 15 mwaka huu.
“Zimbabwe hatimaye inarejea kwenye Jumuiya ya Madola, baada ya barua yao waliyowasilisha ya maombi kufanikiwa itakuwa tukio la aina yake na historia itandikwa,” alisema Scotland.
Mnangagwa anatarajia kutaja tarehe ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, kabla ya kumalizika kwa mwezi huu. Uchaguzi huo unatajwa kuwa kipimo cha kwanza cha Rais huyo kuhusu hali ya demokrasia.
Rais huyo ameahidi kufanyika kwa uchaguzi huru na haki nchini humo.