Nahodha Msaidizi wa Kikosi cha Simba SC Mohamed Hussein Zimbwe Jr, ameweka wazi wamejipanga kusaka ushindi dhidi ya Azam FC, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Simba SC itacheza dhidi ya Azam FC mchezo wao wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kesho Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Beki huyo wa Kushoto amesema moja ya malengo yao kwa sasa ni kuhakikisha wanachukua ubingwa wa ASFC, hivyo wanapaswa kupambana kwa malengo ya kupata ushindi.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, lakini kama wachezaji tumejipanga kupata ushindi ili tusonge mbele, huu ni mchezo muhimu sana kwetu, tunawahidi mashabiki wetu tutapambana kuhakikisha tunasonga mbele na kucheza Fainali ya ASFC.” amesema Zimbwe Jr.
Tayari vikosi vya Simba SC na Azam FC vimewashawasili mjini Mtwara kwa ajili ya mchezo huo, ambao umepangwa kuanza kuunguruma majira ya saa tisa alasiri.
Timu hizo zinakutana huku Azam FC ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0 katika hatua ya Nusu Fainali ya michuano hii msimu wa 2020/21, lililofungwa na mchezaji wake wa zamani, Luis Miquissone baada ya mabeki kuzembea.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma, Miquissone alifunga bao hilo dakika ya 89 baada ya mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Bernard Morrison anayeicheza Young Africans kwa sasa kuanzisha kwa haraka mpira wa kutenga ‘Free-Kick’.