Uongozi wa Klabu ya Real Madrid huenda ukakaa chini na gwiji wa klabu hiyo Zinedine Zidane kumpa kazi kwa mara ya tatu ili achukue mikoba ya kocha Carlo Ancelotti.
Ancelotti amepanga kuachana na miamba hiyo ya Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu huu 2023/24 baada ya kukubali kwenda kuwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil.
Mpango huo unaifanya Real Madrid kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya, lakini Zidane anaendelea kuwa chaguo la kwanza, kwani ameshawahi kuinoa timu hiyo mara mbili tofauti.
Katika awamu zake mbili alizokuwa kwenye timu hiyo, Zidane alishinda La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa, tangu mwaka 2021 hana kazi, lakini uhusiano wake mzuri na rais wa Los Blancos, Florentino Perez unampa nafasi ya kurudi Bernabeu.
Mastaa wengine wa zamani wa Real Madrid wanaopewa nafasi ya kwenda kukinoa kikosi cha Real Madrid ni Xabi Alonso, Raul na Alvaro Arbeloa.
Kwa msimu uliopita, Real Madrid ilishindwa kufanya kweli kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mataji hayo yalinyakuliwa na Barcelona na Manchester City.
Kwenye Ligi ya Maingwa Ulaya, chama hilo la Ancelotti lilikomea kwenye hatua ya Nusu Fainali na kutupwa nje kwa jumla ya mabao 5-1, baada ya sare ya 1-1 uwanjani Bernabeu katika mechi ya kwanza, kabla ya kipigo cha mabao 4-0 katika mechi ya marudiano iliyofanyika Etihad.
Katika kuhakikisha wanakuwa na viwango bora kwa msimu ujao na wanafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali, Real Madrid imeleta nguvu mpya kwenye safu yake ya kiungo baada ya kumsajili Jude Bellingham kutoka Borussia Dortmund kwa pesa nyingi na kumfa nya kuwa Mwingereza ghali.
Madrid imelipa Pauni 115 milioni kupata huduma ya kiungo huyo wa zamani wa Birmingham City.
Mabosi wa Real Madrid wanaamini kwa kutoa ajira kwa mtu anayefahamu vyema falsafa za timu hizo zitawafanya kuendelea kutamba ndani ya uwanja na kubeba mataji, hasa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, taji ambalo wamelichukua mara nyingi kuliko timu nyingine yoyote.