Meneja wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Zinedine Zidane, amesema kikosi chake kitacheza mfumo wa kushambulia dhidi ya FC Bayern Munich, kwenye mpambano wa utakaounguruma uwanja wa Santiago Bernabeu.
Real Madrid watawakaribisha mabingwa hao wa soka nchini Ujerumani katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, huku wakiwa mbele kwa ushindi mabao mawili kwa moja walioupata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa juma lililopita mjini Munich.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ulipofanyika mjini Madrid, Zidane amesema litakua kosa kubwa kwa kikosi chake kucheza mchezo wa kuzuia, kutokana na kuwafahamu vyema wapinzani wao ambao amewatabiria watacheza kwa morari ya hali ya juu.
Meneja huyo kutoka nchini Ufaransa amesema, mfumo wa kushambulia anaamini utakua bora zaidi kutokana na kikosi chake kuhitaji mabao mengine katika mchezo wa kesho, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza mchezo wa fainali mara ya tatu mfululizo.
“Ninatarajia kutumia mfumo wa kushambulia, naamini utatusaidia kufikia lengo la kupata mabao mengine ambayo yatatuwezesha kwenda katika hatua nyingine.
“Mchezo huu bado upo wazi kwa kila upande, hivyo yoyote anaweza kushinda endapo atapambana vizuri, lakini kwa upande wetu tumejiandaa kushinda ili kutimiza lengo la kucheza mchezo wa fainali wa michuano ya Ulaya kwa mara ya tatu.” Amesema Zidane.
Edapo Real Madrid itafanikiwa kutinga fainali, Zidane ataweka rekodi ya kipekee barani Ulaya kwa kufanikiwa kuwa meneja wa kwanza kufanya hivyo mara tatu mfululizo.