Maisha ya binadamu yamejawa na mengi ya kustaajabisha, kuhuzunisha na wakati mwingine hata kukumwaga machozi japo yapo mengi yenye kufurahisha vile vile, kadri tunavyoendelea kuishi, ndivyo tunavyoendelea kuona na kusikia hadithi za watu wengine zinazoweza kutufanya tububujikwe na machozi, yapo ya kututia moyo na wakati mwingine kutufanya tuyaheshimu na kuyathamini maisha tuliyonayo sasa na kila tulichobarikiwa.
Msisimko unaoweza kuzalisha hisia zenye kusimamisha vinyweleo vya ngozi ya mwanadamu yeyote mwenye ubinadamu wa dhati ndani yake, kamwe hautaacha kumpata yeyote atakayekutana uso kwa uso na Zion Zacharia Daniel maarufu Zion Clark.
Huyu ni Kijana mwenye umri wa miaka 21, Mcheza mieleka wa daraja la kwanza, mwanariadha mahiri , aliyeingia kwenye kitabu cha rekodi za Dunia, Guinness World Records, mhamasishaji na mwandishi. Ambaye kwasasa amefanikiwa kupata ukubwa na Dunia inamfahamu, jambo ambalo halikuweza kutokea kirahisi.
Alizaliwa akiwa na tatizo la kiafya ambalo hutokea kwa nadra sana linalojulikana kama ‘Caudal regression syndrome’, hali inayomfanya mtoto kuzaliwa akiwa na upungufu wa viungo fulani mwilini hasa miguu, ambapo kwa mujibu wa daktari Brian Sutterer anaeleza kuwa tatizo hilo humkuta mtoto mmoja kati ya watoto 100,000 wanaozaliwa kwa mwaka Duniani kote.
Tofauti na mazoea ya wengi kuwa yeyote asiye na miguu au upungufu wa viungo fulani mwilini ni mlemavu, Kijana Zion yeye anaipinga vikali dhana hiyo kuliko kitu chochote kwenye maisha yake, kiasi cha kuamua kuishi na kaulimbiu ya ‘NO EXCUSES’ ambayo imetokana na jina kitabu cha Kyle Maynard ambaye ni mmoja wa watu waliomuhamasisha kutokukata tamaa licha ya kupitia magumu kwenye safari nzima ya maisha yake, Mateso, vikwazo, machozi jasho na damu alizomwaga kabla ya kuwa Zion wa leo.
Zion anamtaja mwanamieleka Klye Maynard ambaye ndio mtu wa kwanza mwenye upungufu wa viungo mwilini kama ilivyo kwa Zion, aliyeweka rekodi ya binaadamu wa kwanza tangu dunia kuumbwa aliyefanikiwa kuingia kwenye rekodi ya kuupanda milima mrefu zaidi barani Afrika, wenye urefu wa mita za mraba 5,895 akazikata takribani futi 19,340 moja kwa moja mpaka kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro, Uhuru peak, akiupanda kwa kutumia vipande vya sehemu za mikono yake.
NO EXCUSES yaani hakuna visingizio ameifanya kuwa nembo yake pendwa aliyoamua kuichorea tattoo mgoni kwake kwa maandishi makubwa ikiwa ni sehemu ya kujihamasisha na kuwahamasisha kujikubali na kufanya kinachowezekana kwa kile ulichobarikiwa.
Zion Zacharia Daniels, yeye sio tu binaadamu aliyeweza kuishi bila miguu bali ameweza kuwastaajabisha mamilioni ya watu ulimwenguni, kwa kuwa mpigana mieleka asiye na miguu, aliyefanikiwa kushiriki na kushinda mashindano kadhaa…..Yaani kwa upande mwingine Zion ni sawa na mchezaji wa mpira wa miguu mwenye kucheza kwa miguu yote miwili maana licha ya Mieleka, ni mwanariadha mahiri na mhamasishaji pia.
Zion Zacharia Daniels, alizaliwa Septemba 29,mnamo 1997, huko Columbus, Ohio nchini Marekani, na baada ya kuzaliwa maisha yake yote yalikuwa katika vituo vya kulelea watoto yatima, ambapo inaelezwa aliishi katika vituo saba au tisa hivi.
Hii ni kulingana na makadirio yake mwenyewe. Huko, alikuwa akipitia kila aina ya misukosuko akiwa mtoto mdogo asiye jiweza kwa lolote huku akikabiliana na changamoto nzito ya kutokuwa na miguu.
Zion alipitia nyakati za kushinda na njaa na vipindi vingi vya kupigwa na kunyanyapaliwa, kama ambavyo yeye mwenyewe amekuwa akisimulia.
“Sitasema uwongo, sikuwa mtoto mzuri. Baada ya kila kitu nilichopitia, nilikuwa na mtazamo mbaya sana kwa mambo mengi baada ya matendo niliyofanyiwa, hii ni kutokana na mateso niliyopitia katika makuzi yangu. Alisema Zion wakati akizungumzia kumbukizi za maisha yake ya utotoni.
Mama yake mzazi alipata ujauzito wa Zion akiwa gerezani, alipokuwa akitumikia kifungo, wakati huo alikuwa mgonjwa wa kisukari na muaathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, hivyo kitendo cha yeye kushika mimba pia kilikuwa kama mzigo.
Kulingana na hali halisi ya mama yake hata baada ya Zion kuzaliwa ilionekana kuwa asingeweza kumlea mtoto huyo ipasavyo, hivyo ikal9azimika Zion kupelekwa kwenye vituo vya kulelea watoto yatima ambako alipitia misukosuko mingi kiasi cha kumfanya kuanza kukomaa kiakili akiwa na umri mdogo licha ya kuweka wazi kuwa mapitio hayo kuna wakati yalimuathiri sana kiakili.
“Mama yangu mzazi hakuna kitu alisadia, alikuwa mgonjwa wa kisukari na pia alikuwa akitumia dawa za kulevya, alikuwa mtu wa matukio hivyo alikuwa mara nje mara jela, ni kweli alipata uja uzito akiwa gerezani,na hata baada ya mimi kuzaliwa, ilionekana kuwa hafai kunitunza, kwa hivyo nilienda kwenye nyumba mbili za kwanza kulelewa.
Sio mbaya, lakini mambo kadhaa mabaya yalinitokea, kwa hivyo ilibidi niondolewe sehemu ya kwanza na kwenda nyingine, lakini kulikuwa na nyumba zingine ambako nilikwenda kuishi, ambapo kuna nyakati nilipitia vipindi fulani vya njaa, kunyanyapaliwa na mambo mengi mabaya, lakini nashukuru neema ya mungu wangu. mama yangu Kimberli Hawkins alinishika na iliyobaki ni historia”. Alisema Zion kwenye moja ya mahojiano mnamo mwaka 2019, huko Marekani.
Zion akiwa na miaka 16 alifanikiwa kutimiza ndoto ya kupata mtu wa kumfuta machozi, baada ya kujitokeza mwanamke aliyejitolea kumuondoa kwenye maisha tata ya kulelewa kwenye vituo na kuanza maisha ya kuishi katika mfumo wa familia, mwanamke huyo aitwaye Kimberli Hawkins alimchukua na kwenda kuishi naye kama mama na mwana na kumpa upendo ambao Zion hakuwahi kuupata hata siku moja kwenye maisha yake.
Moja ya ndoto kubwa ya Zion ilikuwa ni kumpata mtu atakayemuita mama na kuishi nyumbani sehemu yeye mfumo wa tufauti na alikokuwa akiishi kwa kipindi kirefu cha maisha yake tangu kuzaliwa kwake.
Kimberli Hawkins huyu ni mwanamke aliyewahi kufanya kazi katika vituo vya kulelea watoto waliokosa malezi ya wazazi wao, na siku zote alikuwa na ndoto ya kupata mtoto wa kiume, lakini bila kujali mapungufu aliyokuwa nayo Zion hakusita kuifanya ndoto yake kuwa kweli, alimchukua na kuanza kumlea upendo, amani na furaha unaoendelea mpaka sasa.
Hawkins alikaririwa akisema kuwa kitendo cha yeye kumchukua Zion ni moja ya mambo makubwa kuwahi kutokea kwenye maisha yake na anajivunia kuwa mama mlezi wa Zion.
licha ya kumpata mama wa kumfuta machozi, inaelezwa kuwa mpaka sasa hakuna historia yeyote ya ziada kuhusu wazazi halisi wa zion walipo.
Kwa takribani miaka 15 maisha yake ya nyuma yalikuwa katika mfumo wa kulelewa kwenye vituo, kipindi chote hicho kilikuwa cha malezi ya mateso na misukosuko kutoka kwa watu waliokuwa wanamzunguka, hali iliyopelekea Zion kuishi kwa kuhama hama kwenye makazi tofauti tofauti.
Ingawa maisha yake yalikuwa magumu, alikataa kata kata kuruhusu tofauti zake za kimwili na hali mbaya ya maisha yake imvunje moyo wa kuendelea kuzipigania ndoto zake. Hivyo baada ya kuanzishwa kwa kipindi cha mchezo wa mieleka katika shule ya aliyokuwa anasoma, hapo walau kila kitu kilibadilika.
Akiwa na umri wa miaka 8, alikutana na mtu muhimu na aliyemthamini zaidi, wa kwanza katika maisha yake, ambaye ni mwalimu wa sanaa na mkufunzi wa mchezo wa mieleka Mr Gil Donahue. Mwalimu huyo alivutiwa na Zion kiasi cha kuanza kumsaidia hata vilipokuwa vikitokea vipindi vya kusumbuliwa au kudhulumiwa na wanafunzi wenzake.
Katika kumfuatilia kwa makini, mwalimu huyo aligundua kuwa Zion alikuwa na kipaji cha kipee na hata kubaini kuwa ndani yake alikuwa ni mwenye mapenzi makubwa na mchezo wa mieleka. kisha akaanza kumjenga kiakili kwa kumtia moyo na kumhamasisha kuanza kujifunza mchezo huo licha ya ulemavu alionao.
Zion aliuchukua na kuanza kuufanyia kazi ushauri wa mwalimu wake, na ndipo akaanza rasmi kuhudhuria kwenye mafunzo ya mieleka, na taratibu akaanza kuwa mjuzi wa namna ya kucheza na kuanza kushindana na wacheza mieleka wengine.
Nilikua nikipigana mieleka tangu nilipokuwa na umri wa miaka nane, nilipata mapenzi na mchezo huo mapema sana, ingawa nilikuwa nikifanya vibaya, niliendelea kuifanyia kazi kwa bidii ili kujua ni jinsi gani ningeweza kushindana na tofauti zangu za kimwili”.
Ndani miaka 22 kama kocha wa mieleka, Gil Donahue alisema hakuwahi kuona mtu yeyote kama Zion.
“kukutana na Zion kulinifanya niiangalie kazi yangu ya kufundisha kwa mtazamo mpya na wa tofauti kabisa,” Donahue alisema.
“Unamfundishaje mtoto asiye na miguu?”.
“Tulimfanyia majaribio mara kadhaa katika maisha yake yote huko Massillon. Tulichunguza na kugundua ni mbinu gani zitamfanya afanikiwe na ni mbinu gani ambazo hasingeweza kuzitumia. Hivyo ilitulazimu kuanza kutumia mazuri yake kuchimba kwa undani mbinu alizoweza kutumia kulingana na hali yake, na ndivyo mtindo wa mieleka wa Zion ulivyozaliwa.” aliongeza Gil Donahue.
Kutokana na kuweka jitihada zake kwenye mchezo huo hatimaye Zion alimaliza shule ya sekondari akiwa na rekodi ya ushindi wa michezo 33- akishindwa michezo 15 pekee, kwenye Mashindano ya Mieleka ya Shule ya sekondari Ohio High School State Wrestling Championships.
Aliendelea kujiboresha zaidi kwenye mchezo wa mieleka na kitaaluma kupitia chuo kikuu cha Jimbo la Kent huku akiendelea kupambania malengo yake mengine kwenye upande wa riadha,….licha ya ubora wake kwenye mieleka, lengo lake kubwa lilikuwa ni kuwa mwanariadha wa kwanza wa Marekani kushindana katika Olimpiki (mieleka) na Paralympiki (mbio za magurudumu) huko Tokyo japani 2020, na alifanikiwa kutimia hilo.
Kabla ya kushiriki kwenye mashindano hayo huko Tokyo, yaani Baada tu, kufanikiwa kuwa mpiganaji mahiri wa mieleka, baadae alienda kujiunga na mashindano ya mbio za walemavu wa kiti cha magurudumu (paralympic) hii ilikuwa baada kukutana na afisa wa Olimpiki ya Walemavu ambaye alimhimiza kujiunga na shindano hilo.
Na kuanzia hapo , Zion aligundua kuwa alikuwa na uwezo mzuri wa kukimbia kiasi cha kuanza rasmi kujihusisha na michezo hiyo hadi kufukia hatua ya kushiriki michuano mikubwa Duniani.
kulingana na hali ya maumbile ya Zion, maswali ya watu wengi ni kuwa Je, Zion anaweza kuwa na mpenzi? kwa kuwa muundo wa maumbile yake unaibua maswali ya kuwa pengine ulemavu wake unaweza kuwa umeathiri sehemu zake za siri.
Maswali haya yanazirudisha kumbukumbu zangu kwenye moja ya misemo ya Wahenga unaokusema ‘Mungu akikupa ulemavu kamwe hawezi kukunyima mwendo’.
Sasa ukweli ni kuwa. Zion hajaoa lakini yuko kwenye uhusiano wa kimapemzi wa dhati na mpenzi wake, mrembo Bodacious Teitei. Hii ni kwa mujibu wa ushahidi unaopatikana kwenye wasifu wa mrembo huyo aliouandika kwenye ukurasa wake wa instagram, ambaye amekuwa akiposti picha na mambo mbali mbali yenye kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na Zion.
Teitei ni mwanamitindo na mbunifu wa maudhui kutoka New York Marekani.
kinachoonekana ni kwamba wapenzi hao walianza kuwa kwenye mahusiano yao rasmi mapema Januari 2021, Ambapo tangu wakati huo, mrembo tei tei amekuwa akiweka picha nyingi za Zion na ameweka wazi kwamba tayari Zion amekutana na familia yake.
Zion Zacharia Daniels amewahi kushinda ubingwa wa jimbo umbali wa 100m na 400m mnamo 2016, na kuwa mkimbiaji wa mbio za viti vya magurudumu mwenye kasi zaidi huko Ohio, akifikia kasi ya kilomita 32 kwa saa. Mapema mwaka Februari 15, 2021, alifanikiwa kushinda na kuingia kwenye rekodi ya dunia ya Guinness, kama mwanariadha mwenye kasi zaidi mwenye kutumia mikono.
Rekodi hiyo aliiweka kutokana na kukimbia umbali wa mita 20 kwa sekunde 4.78 .
Zion anasema “Mambo mazuri yatakuja ikiwa utajitahidi vya kutosha, lazima uamini katika malengo yako ili kuyafanikisha na ujue kuwa wewe ni unafaa vya kutosha kuyafanya yatimie. Hakuna mtu mwingine anayeweza kukuamini ikiwa hujiamini kwanza.
Kuwa na mfumo wa msaada ndio kila kitu, lazima uwe na watu unaoweza kuwategemea kwa namna mbali mbali. Ni vyema kuwa na timu ya watu wenye nia moja kuliko mtu mmoja anayefanya yote peke yake..”