Ukitaka nyaraka zote zinazokuhusu na zisizokuhusu ziwekwe hadharani, jiunge na siasa katika nchi yoyote duniani. Hali hii inatokana na ukweli kwamba nyaraka zako ni silaha muhimu sana hasa kwa wapinzani wako.

Wakati ambapo watanzania wengi wanaonesha imani yao kwa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli wakiamini ni msafi na mchapakazi na kuonekana kama nyumba nzuri ya vioo, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe amerusha jiwe kwenye nyumba hiyo ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe, Zitto Kabwe amesema kuwa Dk. Magufuli sio msafi kama wengi wanavyodhani kwa kuwa wizara ya Ujenzi anayoiongoza ilibainika kufanya ufisadi wa shilingi bilioni 87 ambazo ni sehemu ya shilingi bilioni 252 za miradi ya umeme, barabara na miradi maalum.

Zitto alieleza kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyokuwa chini ya uenyekiti wake, iliihoji wizara hiyo kuhusu kunyofolewa kwa fedha hizo na walikosa maelezo yenye mantiki.

Zitto Kabwe alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema ambaye alipata umaarufu zaidi kutokana na kuibua na kusimama kidete kupinga ufisadi uliobainika kuwa ulifanywa na watendaji wa serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo, Zitto amekuwa akipinga vikali uamuzi wa chama chake hicho cha zamani kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha Ukawa.

Mwaka 2008, Edward Lowassa alihusishwa na ufisadi wa kampuni ya kufufua umeme ya Richmond, iliyobainika kuwa kampuni hewa iliyolipwa mabilioni ya fedha za umma. Kutokana na mapendekezo ya tume maalum ilyoundwa chini ya uwenyekiti wa mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyeme, Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu.

Ne-yo Kutua Kenya Kwenye Coke-Studio Mwaka Huu
Profesa Lipumba Amuunga Mkono Zitto Kabwe