Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi hususani chakula yanazidi kushuka tofauti na tunavyonunua katika kipindi hiki ambacho nchi inapambana kuingia kwenye uchumi wa viwanda.
Katika ukurasa wake wa facebook ameandika kuwa kuna anguko kubwa la mauzo na tunavyonunua bidhaa kutoka nje na kuingiza ndani ya nchi ambalo linatufanya kuzidi kuwa tegemezi
“Wakati Serikali inaimba viwanda, mauzo ya bidhaa zitokanazo na viwanda kwenda nje ya nchi yetu yameshuka sana, mwaka unaoishia Mei, 2016 Tanzania iliuza nje bidhaa za viwanda za thamani ya dola 1.5 bilioni. Mwaka mmoja baadaye Tanzania imeuza nje bidhaa za viwanda za thamani ya dola 0.8 bilioni tu. anguko la mauzo nje la takribani dola 700 milioni sawa na thamani ya Ndege 23 za Bombadier Q400″, amesema Zitto Kabwe
Aidha, Mbunge huyo ameongeza kuwa pesa ambayo serikali inapoteza kwa anguko la mauzo ya bidhaa ndani ya miaka miwili ni nyingi hivyo ni lazima serikali ipange mikakati endelevu ili iweze kunusuru hali hiyo.
Hata hivyo ameongeza kuwa wakati Serikali ikiimba kuibadilisha nchi kuwa ya viwanda, mauzo ya bidhaa zitokanazo na viwanda kwenda nje ya nchi yameshuka ukilinganisha na mwaka ulioisha.