Kitendo cha Mbunge wa Arusha mjini kukaa rumande kwa zaidi ya miezi minne sasa pasipo kupatiwa dhamana kimemfanya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kushindwa kuzuia hisia zake na kutaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwajibishwe
Zitto amedai kuwa kitendo cha Mbunge huyo ambaye ni mwakilishi wa wananchi kunyimwa dhamana ni siasa za ukomoaji ambazo zinajenga chuki kwenye jamii ambapo chuki huwa zinazaa visasi.
“Haitoshi Majaji kukemea Ofisi ya DPP, Mfumo wetu lazima uweke uwezo wa waendesha mashtaka wa aina ya kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini kuwajibishwa. Wanasheria tazameni namna ya kuwajibisha Ofisi ya DPP kwa uonevu wa makusudi dhidi ya wananchi,” amesema Zitto.
Hata hivyo kauli hiyo ya Zitto imekuja baada ya majaji watatu kutoka mahakama ya rufaa kuitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP kuwa makini na kuwataka kuwashikilia watu kwa misingi ya kisheria na kuongeza kuwa haipendezi na haingii akilini mtu kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki ya dhamana.