Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni limesisitiza kuwa bado linamuhitaji kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu ambapo amesema kuwa bado wanamuhitaji Zitto kwa mahojiano na kwamba walipata taarifa kwamba anaumwa.
Agosti 16 mwaka huu, Askari Polisi walifika katika Makao Makuu ya Chama cha ACT- Wazalendo jijini Dar es salaam kwa lengo la kumkamata Zitto Kabwe lakini hawakumkuta.
”Bado tunamuhitaji Zitto kwa ajili ya mahojiano, ila tumepata taarifa alijisikia vibaya akaenda kupumzishwa katika Hospitali ya Aga Khan, kwa hiyo bado uhitaji wetu kwake upo palepale,”amesema Kamanda Taibu
Amesema kuwa Zitto anazo taarifa za kuhitajika Polisi kwani walimwambia msaidizi wake na amewajibu kwamba akipata nafuu ataenda kwa ajili ya mahojiano na jeshi la polisi.
Aidha, wiki iliyopita, askari polisi wakiwa na gari T 863 DFS wakiwa wamevaa nguo za kiraia, walizuia mkutano wa Zitto na Wanahabari aliokuwa anataka azungumzie kuhusu mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es salaam.
Hata hivyo, baada ya kumkosa Zitto katika ofisi hizo, polisi waliamua kuondoka na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu kwa ajili ya mahojiano lakini baadaye alichiwa huru bila kuhojiwa kwa madai kuwa hakuwa muhusika.