Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa anawashangaa sana wanaoongoza katika kumtuhumu kuwa yeye ni kibaraka wa CCM.
Akiongea alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mabawa uliolenga kukitangaza rasmi chama chake kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na vitongoji vyake Zitto alisema katika kipindi alichookuwepo Bungeni ameongoza mapambano ya kuwang’oa mawaziri 13 wa serikali.
“Mwaka 2012 niliongoza mapambano ya kuwang’oa mawaziri wanane wakati mwaka 2013 walijiuzulu mawaziri wanne kwa kashfa ya Oparesheni Tokomeza, wakati mwaka jana, mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walilazimika kuachia ngazi kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta escrow. Wananchi wa Tanga jiulizeni, hivi msaliti anawezaje kuwang’oa mawaziri wote hao ndani ya kipindi cha miaka mitatu?” alihoji Zitto na kusisitiza kuwa kuna watu wamelenga kutumia hoja hiyo kwa lengo la kumchafua.