Mchezaji mkongwe wa AC Milan Zlatan Ibrahimovic, amepata majeraha kwenye mguu wake wa kulia akiwa mazoezini, na huenda ikamchukua siku kumi kurejea tena katika hali yake ya kawaida.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38, alishindwa kuendelea na mazoezi ya pamoja ya kikosi cha AC Milan siku ya jumatatu mjini Milan, na tayari ameshaanza matibabu.
Taarifa iliyotoewa na AC Milan jana Jumanne imeeleza kuwa, mshambuliaji huyo alilazimika kusitisha mazoezi na kukaa pembeni kufuatia jeraha alilolipata.
“Zlatan Ibrahimovic amepatwa na majeraha ya mguu wake wa kulia, anatarajiwa kufanyiwa matibabu kwa siku kadhaa na huenda akarejea mazoezi baada ya siku 10.” Imeeleza taarifa ya AC Milan
Ibrahimovic alirejea AC Milan mwezi Januari na kusaini mkataba wa miezi sita, baada ya kumalizana na LA Galaxy ya Marekani.
Hatma ya ligi ya Italia (Serie A) inatarajiwa kujulikana kesho Al-Khamis, baada ya Serikali ya nchi hiyo kutoa tamko kuhusu mustakabali wa michezo iliyokua inaendelea kabla ya kulipuka kwa maambukizi ya Virusi vya Corona.
Serie A ilisimama Machi 9, kupisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona huku AC Milan, ikiwa inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya Italia ikiwa na alama 36.