Mshambuliaji nguli kutoka nchini Sweden na Klabu ya AC Milan Zlatan Ibrahimovic rasmi ametangaza kustaafu kucheza soka, imeeleza taarifa kutoka mjini Milan, Italia.
Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 na AC Milan unamalizika mwezi huu mwishoni na hautaongezwa tena kufuatia msimu unaokumbwa na majeraha, jambo linalomsukuma kukatisha muda wake wa kucheza.
Lakini Ibrahimovic baadae alifichua katika mkutano na waandishi wa habari hakuna aliyejua kama angeamua hivyo.
“Hata familia yangu haikujua, kwa sababu nilitaka wakati natangaza kila mtu asikie kwa wakati mmoja,” alisema.
Ibrahimovic alifunga mabao 93 katika mechi 163 kwenye misimu miwili akiwa Milan.
Alirejea Januari, mwaka 2020 na kuisaidia Milan kushinda taji la Serie A mwaka jana, taji lake la pili la ligi akiwa na Rossoneri hao.
Mshambuliaji huyo mahiri, ambaye amefunga mabao 561 kwa klabu na taifa katika kipindi chote cha maisha yake ya soka, alitokwa na machozi wakati mashabiki wa Milan wakifunua bango kubwa upande mmoja wakisema “Kwaheri” na kuimba jina lake.
Ibrahimovic alikunja mikono yake kwa umbo la moyo na akapiga busu kwa mashabiki. Pia kulikuwa na sherehe maalum iliyowekwa kwake baada ya mechi, wachezaji na wafanyakazi wa Milan wakimpa ulinzi wa heshima alipokuwa akitoka uwanjani.
“Nawaaga kwa soka,” alisema baada ya kushangiliwa na umati wa watu wa San Siro kufuatia ushindi wa Milan wa mabao 3-1 dhidi ya Hellas Verona katika mchezo wao wa mwisho wa ligi.
Mshambuliaji huyo alianza soka lake la kulipwa katika klabu ya Malmo FF mwaka 1999 na aliondoka kwenda Ajax Amsterdam 2001 kabla ya kuanza maisha yake ya soka ambayo yamejumuisha timu za Ulaya zikiwamo Manchester United, Paris Saint-Germain, Inter Milan na AC Milan.
Ibrahimovic alikuwa na majeraha na alicheza mechi nne pekee msimu huu akiwa na Milan, baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwaka jana.