Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic amewahakikishia waandishi wa habari kuwa na furaha ya kuendelea kuitumikia klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint Germain licha ya kuelezwa wazi anaweza kusaka mahala pengine pa kucheza soka lake msimu ujao wa ligi.

Zlatan aliwaeleza waandishi wa habari maneno hayo akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa lake ambayo inajiandaa na michezo ya kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya dhidi ya Urusi pamoja na Austria.

Mshambuliaji huyo mwenye kaliba ya kusaka mafanikio kila anapokwenda, amesema haikuwa mshangao kwake alipoambia anaweza kuondoka kwenye klabu ya PSG kutokana na kufahamu wazi maisha ya soka namna yalivyo.

Amesema suala la kuhitajika kwenye klabu ya AC Milan ya nchini Italia ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kuelekea nchini Ufaransa kujiunga na PSG alilipokea kwa furaha na kukwama kwa mpango huo baada ya dirisha la usajili kufungwa hakujamuumiza zaidi ya kuangalia namna gani anaweza kuisaidia PSG ili itete ubingwa wake msimu huu.

Zlatan amesisitiza kuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa PSG na kuambiwa wazi jambo la kupewa uhuru wa kuondoka klabuni hapo haikumaanisha kama palikua na ugomvi ambao ulisababisha kauli hiyo kutolewa na walio juu yake.

Hata hivyo amedai kwamba kutokana na umri wake kwa sasa anajua changamoto ua kupambana na vijana wanaoendelea kuchipukia duniani pamoja na kwenye klabu ya PSG huenda ukawa kikwazo japo anaamini bado ana uwezo mkubwa wa kupambana.

Zlatan kwa sasa ana umri wa miaka 33 na tayari uongozi wa PSG umeshaonyesha dhamnira ya kupangua safu yake ya ushambuliaji kwa kutaka kuwasajili wachezaji wengine kitakapofika kipindi cha majira ya baridi (mwezi Januari/ dirisha dogo).

Mbali na klabu ya AC Milan kutajwa kuwa na mkakati wa kumsajili Zlatan, pia klabu za Arsenal pamoja na Fenerbahce na Galatasaray zote za nchini Uturuki zinatajwa kuwa na mpango wa kumsajili.

Marotta: Thamani Ya Pogba Ilikua Euro Milion 100
“Lowasa: Nitapambana Na Ufisadi Kwa Kasi Ya Ajabu”