Kocha Mkuu wa Young fricans Zlatko Krimpotic mapema hii leo Agosti 29 aliwasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kukinoa kikosi cha klabu hiyo ambacho kilianza mazoezi Agosti 10.

Raia huyo wa Serbia anachukua mikoba ya Luc Eymael ambaye alifutwa kazi Julai 27 baada ya kutoa lugha za kiubaguzi.

Anaungana na Juma Mwambusi ambaye ni kocha msaidizi, ambapo tayari alishaanza kazi ya kukinoa kikosi hicho Uwanja wa Chuo cha Sheria jijini Dar es salaam.

Zlatko amepewa kandarasi ya miaka miwili kukinoa kikosi hicho chenye maskani yake Jangwani na kwa sasa kinajiandaa kwa ajili ya Wiki ya Mwananchi ambapo kilele chake ni kesho Agosti 30, Uwanja wa Mkapa.

Siku hiyo ni rasmi kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wapya na wale ambao walikuwa na kikosi kwa msimu wa 2019/20.

Hata hivyo, hofu imeanza kutanza kwa wadau wa soka nchini kuhusu muda wa miaka miwili ambao kocha huyo amekubali kufanya kazi akiwa na Young Africans kwa mujibu wa mkataba wake atakaousaini mara baada ya kuwasili jijini Dar es salam.

Wadau wa soka wanahisi huenda kocha Zlatko akashindwa kumaliza kipindi hicho hasa kutokana na rekodi yake ya kutodumu kwa muda mrefu katika klabu moja.

Katika klabu 19 alizozifundisha ni Degerfors IF ya Sweden pekee ambayo alidumu nayo kwa kipindi kirefu kuanzia 1994–1996 na zingine 18 alizozinoa amekuwa akifanya kazi kwa mwaka mmoja ama pungufu ya hapo kabla ya kuachana nazo.

Beki huyo wa zamani wa Yugoslavia, Zlatko ambaye kwa sasa ana miaka 62, aliichezea timu hiyo ya taifa michezo minane kati ya mwaka 1980–1982 na timu yake ya kwanza kuinoa ilikuwa Degerfors IF kati ya mwaka 1994–1996, kisha akaifundisha loga Jugomagnat ya Macedonia, mwaka 1997–1998, kabla ya 1999 kuino Ankaragücü (Uturuki) na baada ya hapo mwaka 1999–2000 akatimkia OFK Beograd ya Serbia.

Mwaka 2000 akainoa Obilić ya Sebia kisha 2001 akaifundisha Paniliakos ya Ugiriki na mwaka huo huo akatimkia Nea Salamis ya Cyprus kabla 2002 kujiunga na Kairat ya Kazakhstan.

Mwaka 2005, Zlatko aliteuliwa kuwa Kocha wa U-17 wa Serbia and Montenegro na kipindi cha 2005–2006 akainoa Kazma ya Kuwaiti wakati 2007–2008 akirejea Serbia na kukinoa kikosi cha U-19.

Kituo kilichofuata kwa kocha huyo kilikuwa OFK Beograd ya Serbia akifanya kwa muda mfupi na kuondoka kisha mwaka 2014 akarejea tena kabla ya 2015 kuanza kufanya kazi Afrika kwa mara ya kwanza kwa kuwa kocha msaidizi wa Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.

Baada ya hapo kitua kilichofuata kwa kocha huyo kilikuwa Don Bosco ya Haiti mwaka 2016 kisha akarejea Afrika wakati huu akitua ZESCO United (Zambia) mwaka 2017 na mwaka uliofuata akatimkia Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Kituo kilichofuata kwa Zlatko kilikuwa APR FC ya Rwanda 2019 ambako mwaka huo huo akatimkia Polokwane City ya Afrika Kusini kabla ya sasa kujiunga na Young Africans.

"Msiseme tu Magufuli ameshinda..."
Wanaofanya ujangili kipindi cha kampeni watahadharishwa