Kazi ya kumaliza tatizo la pumzi kwa wachezaji wa Young Africans, imeanza kufanywa na benchi la ufundi la klabu hiyo chini ya kocha kutoka nchini Serbia Zlatko Krmpotic, ambaye alikiri kubaini changamoto hiyo mara baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Jumapili Septemba 06.

Young Africans wameanza maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 dhidi ya Mbeya City utakaochezwa mwishoni mwa juma hili, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Zlatko amesema kazi kubwa anayoifanya katika kipindi hiki cha kuelekea mpambano dhidi ya Mbeya City, ni kuhakikisha wachezaji wanakua ‘fiti’ kwa hali zote, ili changamoto ya pumzi isijirudie tena.

“Wachezaji wangu wanajituma na wanafanya vizuri, nimegundua kwamba tatizo lipo kwenye pumzi na imetokana na kutofanya maandalizi ya muda mrefu, bado tuna muda wa kufanya vizuri, makosa yaliyopo tutayafanyia kazi.” amesema Zlatko.

Amesema anaamini baada ya maandalizi ya siku kadhaa ndani ya juma hili, kikosi chake kitashuka dimbani kuikabili Mbeya City kikiwa tofauti, na anaamini wataondoka na matokeo mazuri.

“Nina imani kila tunavyoendelea kucheza, kikosi kitakuwa kinaimarika, ninaona pia wachezaji wameanza kuzoeana na kuimarika zaidi,” amesema kocha huyo.

Katika hatua nyingine kocha Zlatko amesema hana tatizo kwenye safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa Mghana, Michael Saporng ambaye alifunga bao la kusawazisha katika mchezo wao uliopita.

Urusi yaogopa vikwazo vya G7
Mambo bado magumu- Lissu

Comments

comments