Wachezaji wazawa wa Young Africans wametajwa kuwa sababu ya kushindwa kufikia lengo la kuanza vyema Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, dhidi ya Tanzania Prisons juzi Jumapili Septemba 06 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo Young Africans waliambulia sare ya kufunga bao moja kwa moja dhidi ya maafande hao kutoka jijini Mbeya, ambao msimu huu wamehamisha makazi yao kwa muda na kuyapeleka mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Lawama kwa wachezaji wazawa zimetolewa na kocha mkuu wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Zlatko Krmpotic, ambapo amesema tatizo aliloliona ni pumzi kwa wachezaji hao.

Hata hivyo Kocha Zlatko alifanya mabadiliko makubwa kwa kuwaingiza Wakongomani Tuisila Kisinda na Mukoko Tunombe pamoja na mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Sogne Yacouba, wakati wa kipindi cha pili, lakini bado matokeo yakabaki sare ya moja kwa moja.

“Wachezaji wazawa hawakuwa fiti kuweza kucheza kwa dakika zote 90, hata hawa wageni walielezwa programu ya mchezo muda mfupi kabla ya mechi,” amesema Zlatko.

Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Young Africans, Juma Mwambusi, alitetea kauli hiyo ya bosi wake akieleza alimaanisha kwamba alikuwa na muda mfupi wa kusoma uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

“Hakuwa na maana hiyo, alimaanisha bado hajapata muda wa kutosha kumsoma mchezaji mmoja mmoja na si kuhusu ‘fitness’ ya wachezaji wazawa,” Mwambusi alifafanua.

Aidha, Zlatiko amesema baada ya matokeo ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, atahakiksha anafanyia kazi mapungufu yaliojitokeza katika mchezo uliopita, na sasa wanahitaji kufanya vizuri na kuondoka na alama tatu muhimu dhidi ya Mbeya City.

Juzi Jumapili, Kocha Zlatko alifanya maamuzi ya kutumia wachezaji wote wazawa isipokuwa mshambuliaji wa kati tu, Michael Sarpong kutoka nchini Ghana, na ndipo alipobaini tatizo la pumzi.

Young Africans watarudi tena dimbani mwishoni mwa juma hili, kwa kuwakaribisha Mbeya City FC Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na huenda mchezo huo ukawa na mtazamo tofauti kwa upande wa timu hiyo yenye maskani yake makuu kwenye makutano ya Twiga na Jangwani.

Mbeya City FC walianza vibaya Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana Jumatatu kwa kukubali kufungwa mabao manne kwa sifuri na KMC FC, Uwanja wa Uhuru Dar es salaam na kuwa timu ya kwanza kuruhusu kufungwa mabao mengi msimu huu 2020/21.

Waliomuua Khashoggi kwenda jela miaka 20
JPM: Kitwanga alinisumbua