Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza rasmi kuwa Agosti 23, 2022 ni tarehe ya zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo itakua ni siku ya Jumanne.

Rais Samia amesema kuwa serikali imewasikia viongozi wa dini mbalimbali walioomba siku hiyo isiwe siku ya ibada ili watu wote washiriki zoezi hilo.

Ameomba changamoto za kimila na desturi zisiwe chanzo cha watu kutokubali kuhesabiwa ili taarifa za watu wote zifike kwa usahihi.

“Tuna changamoto za kimila na desturi ndani ya jamii yetu, kuna wanaoamini kuhesabiwa ni balaa na nuksi, serikali isingependa kusikia asilimia ya watu haikuhesabiwa. Hii si nzuri sana kwenye ripoti zetu, tunahesabiwa kwa huduma za uchumi na maendeleo, hakuna sababu nyingine iliyojificha nyuma ya pazia. Serikali haiwezi kupanga mipango ya maendeleo bila takwimu sahihi za watu.” amesema Rais.

Mbali na kutangaza Tarehe halisi ya Sensa, Rais Samia akiwa pamoja na Rais wa Zanzibar amezindua nembo itakayotumika katika shughuli za sensa kwa mwaka huu na ameagiza nembo hiyo itumike kwa shughuli zote za kiserikali na taasisi binafsi ili kuhamasisha wananchi waweze kutambua umuhimu wa kihesabiwa.

“Kwa taasisi za Serikali nembo hii iwekwe kwenye machapisho, website na mitandao ya kijamii lakini kwa upande wa taasisi binafsi zinaweza kuwekwa hata kwenye vifungashio au risiti na tiketi, kikubwa kila sehemu tuone hiyo nembo,” amesema Rais Samia.

Awali Mwenyekiti wa kamati ya sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema siku ya sensa imepangwa kwa kuzingatia maombi ya viongozi wa dini isiwe siku ya ibada.

Majaliwa amesema mpaka sasa maandalizi ya shughuli hiyo ya sensa yamefikia asilimia 79 na kwamba kazi hiyo inaendelea kuratibiwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali zote mbili; Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Tukio la uzinduzi wa nembo ya sensa ya watu na makazi umefanyika Golden Tulip Hotel, Zanzibar.

ASFC: Simba Vs Pamba FC yapigwa kalenda
Utata wa Abdi Banda, Mtibwa Sugar wakaa kimya