Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki, amepongeza hatua ya Uongozi wa klabu hiyo kupata Michezo ya Kimataifa ya Kirafiki kupitia Michuano maalum itakayopigwa mjini Omdurman-Sudan.
Klabu ya Al Hilal imeialika Simba SC kwenye Michuano hiyo iliyoanza jana Jumanne (Agosti 23), katika kipindi hiki cha mapumziko kupisha Michezo ya Kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’.
Kocha Zoran amesema Michezo hiyo miwili itakisaidia kikosi chake kuwa katika hali nzuri ya kiushindani, kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema upande wa Michuano ya Kimataifa itawajenga katika njia mbili tofauti, ya kwanza ni utayari wa kwenda kupambana na yoyote na ile ya pili ni kujenga utayari wa kucheza ugenini hasa ukizingatia watanzia nchini Malawi dhidi ya Nyasa Big Bullet.
“Simba tunakwenda kucheza Michezo ya Kimataifa na aina ya timu zenye mtazamo wa kiushindani, ninaamini ushindani tutakaoupata dhidi ya Al Hilal na Asante Kotoko itatujenga vizuri kwa ajili ya Michezo ya Kimataifa na ile la Ligi Kuu.”
“Pia itatujengea uwezo wa kucheza ugenini kwenye Michuano ya Kimataifa kwa sababu tunaanzia ugenini dhidi ya Nyasa Big Bullet, hata tukifanikiwa kuvuka katika hatua zinazofuata bado itatusaidia tutakapocheza ugenini.”
Kocha huyo kutoka nchini Serbia amesema ataondoka nchini na wachezaji wachache wa Kikosi chake, kufuatia wengine tisa kuitwa kwenye Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na Mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa Jumamosi, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
“Sitakua na wachezaji wote ila ninaamini wale waliopo kwenye timu ya taifa wanapata mazoezi ya kutosha na ya ushindani katika michezo hiyo miwili dhidi ya Uganda, wakirudi watakua levo moja ya utimamu wa mwili na hali ya ushindani kama hao nitakaokuwa nao Sudan.” amesema Kocha Zoran
Kwenye Michuano hiyo, Simba SC itacheza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana Agosti 28, kisha itapapatuana na wenyeji Al Hilal Agosti 31.
Tayari Al Hilal imeshacheza dhidi ya Asante Kotoko jana Jumanne (Agosti 23) na kuibuka na ushindi wa 2-0, mabao yakifungwa na Lamin Garjo na Khaki Wad wote raia wa Sudan.
Al Hilal ni mojawapo ya Klabu ambazo huenda zikakutana na Young Africans ya Tanzania kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya kwanza.
Mshindi wa mchezo kati ya Young Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini atacheza na mshindiwa mchezo kati ya Al Hilal dhidi ya St George ya Ethiopia kwenye Mzunguuko wa kwanza.