Beki kutoka DR Congo na Klabu ya Wydad Casablanca Arsene Zolla amekiri kikosi chao kina kazi kubwa ya kupambana dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kesho Jumamosi (Desemba 09) Simba SC itakuwa mgeni wa Wydad Casablanca katika uwanja wa Marrakesh-Morocco, katika harakati za kuwania alama tatu za Hatua ya Makundi, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Beki huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Wydad Casablanca ambacho kiiondoa Simba SC kwenye hatua ya Robo Fainali msimu uliopoita, amesema mchezo dhidi ya wawakilishi hao wa Tanzania siyo rahisi kutokana na mabadiliko ya kikosi cha wekundu hao.
Zolla amesema, Simba SC sio timu rahisi kutokana na wachezaji walionao kwenye kikosi chao ambao wengi ni wale wenye uzoefu mkubwa na michuano kama hiyo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Beki huyo amemuelezea kiungo Fabrice Ngoma kama ingizo muhimu ndani ya Simba SC na kwamba Mkongomani huyo ni mchezaji anayejua vyema soka la Wydad baada ya kuichezea Raja Athletic.
“Unakumbuka tulivyocheza nao huku mara ya mwisho walionyesha mchezo mkubwa lazima unapokwenda kukutana na timu kama hiyo mnatakiwa kuwa makini” amesema Zolla.
“Wana wachezaji waliokomaa sana na mashindano kama haya na unaona sasa wamemuongeza ndugu yangu Fabrice (Ngoma) ni mchezaji mkubwa tunamjua na anaijua Wydad utaona kwamba timu yao sio mbaya.
Aidha Zolla ameongeza hatua ya kikosi cha Wydad kushinda mabao 3-1 jana Ahamis (Desemba 07) mechi ya Ligi Kuu mbele ya Mouloudia Oujda, ni hatua nzuri ya kujiandaa na mchezo huo wa kesho Jumamosi wakiwa na morali.
“Tulikuwa hatujashinda mechi nne mfululizo, lakini sasa angalau tumepata nguvu kuikabili Simba SC.”