Aliyekua Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki amekalia kuti kavu katika klabu Al Ittihad, ambayo ilimshwishi kuondoka Dar es salaam-Tanzania siku chache baada ya kuanza kazi Msimbazi.
Kocha Zoran Maki alianza kazi Klabuni hapo siku chache baada ya kuondoka Simba SC mapema mwezi Septemba 2022, huku akipewa matumaini makubwa ya kuifikisha mbali klabu ya Al Ittihad inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.
Hata hivyo mambo yamemwendea ndivyo sivyo, kwani hadi sasa ameshakiongoza kikosi chake katika Michezo Sita, akipoteza Mitatu na kutoa sare Mitatu, hali ambayo inaifanya klabu hiyo kushika nafasi ya Sita kwenye Msimamo wa Ligi Kuu ya Misri.
Kutokana na hali hiyo Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Al Ittihad imekutana na Kocha huyo kutoka nchini Serbia, baada ya kupoteza mchezo wake watatu dhidi ya Al Ahly mwishoni mwa juma lililopita na kumpa Sharti maalum.
Sharti alilopewa Kocha Zoran ambaye aliwahi kutamba na klabu za Primeiro de Agosto (2017–2019), Wydad AC (2019–2020), Al-Hilal Club (2020–2021) na CR Belouizdad (2021), ni kuhakikisha anashinda michezo mitatu ijayo ili kubadilisha mambo au kufungashiwa virago na kuondoka.
Kabla ya kuondoka Simba SC Zoran aliiongoza Simba SC katika Michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold FC akishinda mabao 3-0 na kisha Kagera Sugar akishinda 2-0.
Kabla ya hapo alipoteza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans iliyochomoza na ushindi wa 2-0, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.