Mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg ameliomba radhi bunge la Marekani kutokana na kushindwa kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao huo.
Mark Zuckerberg, ameliomba radhi bunge hilo kutokana na kushindwa kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao huo kupitia kampuni ya ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica na pia nia ya Warusi ya kuvuruga uchaguzi wa Marekani.
Aidha, katika mahojiano na bunge yaliyodumu kwa saa tano, Zuckerberg ameomba msamaha kutokana na makosa hayo ya Facebook na kuweka wazi kuwa kampuni yake ilikuwa ikishirikiana na mshauri maalumu, Robert Mueller katika uchunguzi wa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.
Hata hivyo, kuhusiana na uchunguzi wa serikali dhidi ya Urusi kuingilia uchaguzi, ambao umechukua nafasi kubwa katika miezi kadhaa, amesema hakuwahi kufanyiwa mahojiano na timu ya mshauri maalumu Mueller, lakini amesema anajua kuwa wanafanya kazi pamoja, ingawa hakuelezea kwa kina zaidi, kulingana na umuhimu kuhusu kanuni za usiri wa uchunguzi huo.