Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi anaodaiwa kuufanya miaka ya 1990 kupitia manunuzi ya silaha.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 75, mapema leo amefika katika Mahakama Kuu iliyoko Durban ambapo alitumia dakika 15 kabla ya kesi yake kuahirishwa hadi Juni 8 mwaka huu.
Zuma anashtakiwa kwa makosa 16 yanayohusishwa na ufisadi, matumizi mabaya ya fedha, kugushi nyaraka pamoja na utakatishaji fedha ambayo yalimtesa wakati akiwa rais. Mashtaka hayo yaliyokuwa yametupwa awali yalirejeshwa tena mahakamani.
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, Zuma alizungumza na wafuasi wake ambao walikuwa wamefurika katika maeneo ya jiji la Durban kumuunga mkono. Alisema kinachofanywa sasa kinashinikizwa kisiasa kwani hajawahi kuona kesi inatupiliwa mbali na baadaye inaanza upya katika mahakama hiyo hiyo.
“Sijawahi kuona daima ambapo mtu anashtakiwa kwa makosa ya jinai, mashtaka yanatupiliwa mbali na mahakama halafu baada ya miaka kadhaa yanarejeshwa tena. Haya ni mashinikizo ya kisiasa tu,” alisema kwa lugha ya Zulu.
Zuma alilazimika kujiuzulu nafasi ya urais baada ya kushinikizwa na chama chake cha ANC baada ya kukumbwa na kashfa nyingi za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.