Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema uamuzi wa masuala yanayohusu chama hicho hayafanywi na mtu mmoja.
Dkt. Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua tawi jipya la CCM katika kata ya Bumbwisudi, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema kuwa masuala yote ndani ya chama hicho yanapaswa kufanywa kupitia vikao husika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na kwamba hakuna kiongozi yeyote ambaye anafanya maamuzi ya chama kwa matakwa yake. Hivyo, aliwataka wananachama katika tawi hilo kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu wa kufanya maamuzi kupitia vikao halali na sio vinginevyo.
Awali, Rais Shein ambaye anaendelea na ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo alitembelea na kukagua mradi wa visima vya maji safi na salama vilivyoko eneo la Bumbwisudi, ambapo kisima kimojawapo kina uwezo wa kutoa lita 220,000 za maji safi na salama kwa saa moja.
Kisima hicho ambacho ni kati ya visima nane vilivyochimbwa katika eneo hilo vikiwa na uwezo tofauti wa kutoa maji safi na salama, ni sehemu ya mradi unaotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Rais Shein aliwataka wasimamizi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika Januari mwakani kuhakikisha wanakamilisha haraka manunuzi ya vifaa vitakavyotumika kufunga mabomba yatakayosambaza maji kwa wakaazi wa mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Mjini Magharibi kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa ahadi za Serikali zilizoainishwa kwenye Ilani ya CCM.
Rais Shein alianza ziara yake mkoani Magharibi Agosti 19 akikagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo. Ziara hiyo itakamilika kesho kwa kutembelea miradi mbalimbali katika wilaya ya Magharibi ‘B’.