Jumla ya Vijana 67,299 waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa mujibu wa sheria katika kipindi cha miaka mitatu (2019 – 2021), 147 kati yao wamekutwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), sawa na asilimia 0.22.
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Februari 3, 2023 iliyowasilishwa na Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Massare imeyasema hayo huku ikieleza kuwa hali ya maambukizi mapya ya VVU ni mbaya licha ya kila mwaka kuonekana inapungua.
Amesema, “kwa kipindi cha miaka mitatu, yaani 2018 hadi 2021, Jeshi la Kujenga Taifa limechukua vijana kwa mujibu wa sheria ambapo vijana wenye Virusi vya Ukimwi katika Jeshi la Kujenga Taifa wanapatiwa huduma mbalimbali kama vile ushauri nasaha kabla ya kupimwa VVU.”
Kufuatia hali hiyo, Kamati hiyo imependekeza mkakati wa kupima na kuzuia maambukizi mapya ya VVU uongezwe huku ikitaka kuchukuliwa kwa juhudi za makusudi za utoaji wa lishe kwa wafungwa wenye maambukizi.
Mwaka 2019, vijana waliojiunga JKT ni 20,413 na 60 kati yao wakikutwa na maambukizi wakati 2020 waliojiunga walikuwa 21,383 na vijana 45 kukutwa na maambukizi huku mwaka 2021 waliojiunga wakiwa ni vijana 25,503 na waliokutwa na VVU wakiwa ni 42.