Klabu ya Chelsea imemtangaza meneja kutoka nchini Ujerumani Thomas Tuchel kuchukua jukumu la kuwa mkuu wa Benchi la Ufundi la klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England.
Tuchel ametangazwa kuchukua nafasi hiyo, baada ya kutimuliwa kwa gwiji wa Chelsea Frank Lampard, ambaye alilazimika kusitishiwa mkataba wake juzi jumatatu, kufuatia changamoto ya kupata matokeo ya kutoridhisha.
Lampard anaondoka klabuni hapo akiwa na zigo la lawama, baada ya kutumia fedha nyingi katika kuboresha kikosi cha Chelsea wakati wa usajili wa majira ya kiangazi, akiwasajili Timo Werner na Kai Havertz, Hakim Ziyech, Ben Chilwell, na Edouard Mendy.
Wachezaji hao kwa pamoja walilipiwa ada kubwa ya usajili ambayo inatajwa kufikia Pauni milioni milioni 222, huku beki kutoka nchini Brazil Thiago Silva akisajiliwa klabuni hapo kama mchezaji huru.
Tuchel atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anairejesha Chelsea kwenye mstari wa ushindi, ili kufikia lengo la kumaliza Ligi Kuu ya England ikiwa nafasi za juu kama si kutwaa ubingwa.
Meneja huyo Mjerumani anajiunga na The Blues huku akiwa na kumbukumbu ya kufutwa kazi na mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain ‘PSG’ mnamo Disemba, lakini anatarajiwa kuwa na mazingira mazuri ya kazi akiwa jijini London, hasa kufuatia uwepo wa wachezaji wenye kiwango cha kimataifa.
Klabla ya kujiunga na PSG na kuambulia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Ufaransa, alitumia misimu saba kufundisha katika Bundesliga, kwanza na Mainz, ambapo aliwaongoza kwenye Europa League, na kisha kipindi cha mafanikio na Borussia Dortmund ambapo alishinda Kombe la Ujerumani.
Akiwa Chelsea, anaungana tena na Christian Pulisic na Thiago Silva ambao aliwafundisha wakati wake huko Dortmund na PSG.