Msanii wa Muziki wa Kizazi kipya Nassib Abdul ‘Dimond’ amekua sehemu ya kuwahimiza mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba SC kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kwa ajili hya kusihangilia timu yao kwenye michuano ya Simba Super CUP inayoanza rasmi leo Jumatano Januari 27.
Diamond amechukua jukumu hilo alipokutana uso kwa macho mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba Haji Sunday Ramadhan Manara alipofika ofisini kwake leo asubuhi.
Msanii huyo amewahimiza mashabiki kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa bila kukosa, ili kuwapa nguvu wachezaji wa Simba SC, watakapokua wakicheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwenye mchezo ambao utaanza mishale ya saa kumi na moja jioni.
Amesema kama mashabiki na wanachama wa Simba SC watajitokeza kwa wingi kwa namna ilivyozoeleka, kuna uwezekano mkubwa kwa timu ya Simba kushinda michezo yao yote miwili na kubakisha ubingwa wa michuano ya Simba Super Cup nyumbani.
Simba itacheza dhidi ya Al Hilal leo Jumatano (Januari 27), kisha itakutana na TP Mazembe siku ya Jumapili (Januari 31) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
TP Mazembe ambao wamewahi kutwaa ubingwa wa Afrika mara tano (1967, 1968, 2009, 2010 na 2015) pia watacheza dhdi ya Al Hilal ya Sudan, keshokutwa Ijumaa (Januari 29).
Michuano ya Simba Super Cup imeanzishwa na klabu ya Simba SC kwa ajili ya kupasha misuli moto kabla ya kuanza kwa nginja ngija za hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwezi Febriari.
Simba SC imepangwa kundi A dhidi ya Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo pamoja na El Mereikh ya Sudan.
Tp Mazembe na Al Hilal wamepangwa Kundi B na CR Belouizdad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.