Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Etienne Ndayiragije amesema mchezo wa mwisho wa kundi D dhidi ya Guinea ni kama fainali, hivyo atawahimiza wachezaji wake kupambana bila kuchoka.
Taifa Stars itatupa karata yake ya mwisho leo usiku saa nne kwa saa za Afrika Mashariki, na kama itafanikiwa kuifunga Guinea itakata tiketi ya kucheza Robo Fainali ya michuano ya ‘CHAN’ kwa mara ya kwanza.
Ndayiragije amesema wachezaji wake watajitoa kwa ari kubwa ya kupambana na anaamini matokeo yatakua mazuri upande wa Taifa Stars, kutokana na maandalizi aliyoyafanya.
“Tunaenda kujitoa kwa sababu ni kama fainali kwetu, nimewaandaa wachezaji wangu kukabiliana na Guinea ambayo ina wachezaji wazuri, lakini nimejizatiti kwa kutumia mfumoa mbao utawabana vilivyo,”
“Lengo kuu ni kupata ushindi katika mchezo huu, ndio maana nimewahimiza wachezaji wangu wacheze kwa kujitoa pasina kuchoka, ili wafanikishe lengo la kuvuka hatua hii ya makundi.” Amesema Etienne Ndayiragije.
Taifa Stars itaingia dimbani leo usiku ikiwa na alama tatu kibindoni walizozivuna kwa kuifunga Namibia bao moja kwa sifuri, huku wakipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Zambia kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri.
Guinea ambao tayari wameshashuka dimbani mara mbili, wamejikusanyia alama nne, baada ya kuichabanga Namibia mabao matatu kwa sifuri na kisha kulazimishwa sare dhidi ya Zambia.